Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto'o amewashukia nyota wa timu hiyo ambao walizaliwa nje ya Afrika kuwa hawachezi kwa kujituma jambo linalopelekea mwenendo usioridhisha ilionao kwenye fainali za Afcon mwaka huu huko Ivory Coast.
Kichapo cha mabao 3-1 ambacho Cameroon ilikipata kutoka kwa Senegal, Ijumaa, kimeiweka katika hofu ya kushindwa kutinga hatua ya 16 bora kwani sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi C ikiwa na pointi moja na inalazimika kuibuka na ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Gambia na kuiombea nuksi Guinea ili iweze kusonga mbele.
Eto'o ambaye aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Cameroon, alisema wachezaji hao ambao wamezaliwa nje ya Afrika, hawajitumi na kujitoa kwa ajili ya timu yao jambo ambalo limechangia ifanye vibaya licha ya ukubwa wake kwenye soka nchini.
"Kaka zangu, nafahamu kuwa wengi wenu hamjazaliwa Cameroon na hamjawahi kuzichezea klabu za Cameroon. Cameroon inapitia kipindi kigumu kwa sababu mapenzi ya nchi ya wazazi hayapo kwa asilimia 100.
"Samahani kwa kujiongelea mimi mwenyewe. Naweza kucheza mechi mbili kwa siku moja kwa mapenzi niliyonayo kwa nchi yetu nzuri. Nilifanya hivyo, Roger Milla alifanya na François Omam Biyick alifanya.
"Mnaamini kwamba Cameroon inatulipa zaidi ya klabu zetu? Hatupati hata 1/10 ya tunachopata kwingine. Ninachokumbuka kutoka kwenu ni tumefanya makosa kuwaleta nyinyi kucheza kwa ajili ya bendera yetu.
"Lakini baada ya Afcon mambo yatabadilika. Tutafanya mtihani wa kupima uzalendo kabla ya kuamua vijana wadogo wachezee timu ya taifa," alisema Eto'o.
Hii sio mara ya kwanza kwa Eto'o kuwakaripia mastaa wa Cameroon ambapo mara ya kwanza alifanya hivyo katika mechi ya kuwania kufuzu mashindano hayo dhidi ya Burundi ambapo alisema atawatimua na kuwatumia wachezaji wa kikosi cha vijana.