Jose Mourinho amesema njaa ya mataji inayomkabili straika Harry Kane ingekwisha miaka mitatu iliyopita endapo kama Tottenham Hotspur ingechagua kumbakisha kwenye benchi la ufundi la timu hiyo.
Kocha huyo Mreno aliyejipachika mwenyewe jina la The Special One, alionyeshwa mlango wa kutokea na bosi wa Spurs, Daniel Levy siku sita kabla ya timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2021.
Spurs iliishia kuchapwa na Manchester City kwenye fainali hiyo na hivyo kuzidi kuendeleza ukame wa mataji kwa straika Kane.
Na licha ya kwamba straika huyo kuchagua kwenda kujiunga na Bayern Munich, ambayo ni wakali wa kubeba mataji, jambo hilo limekuwa tofauti kabisa kwa msimu uliopita baada ya miamba hiyo ya Ujerumani kutoka patupu na kuendeleza njaa ya mataji kwa Kane.
Lakini, Mourinho, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa kocha mpya wa Fenerbahce ya Uturuki alisema: “Kane ameifungia mabao ya kutosha Tottenham na England na bila shaka ataendelea kuifungia mabao Bayern.
Ni mchezaji mzuri na anafunga mabao. Kingine si mchoyo anapokuwa uwanjani, anatoa asisti, anarudi chini kukaba na kuanzisha mashambulizi.
“Kitu pekee anachokosa ni kushinda mataji. Alikuwa mchezaji wangu pale Tottenham na ningeshinda naye taji moja kama nisingefukuzwa siku sita kabla ya mechi ya fainali.”
Kane, 30, matumaini yake ya ubingwa kwa mwaka huu yamebaki kwenye timu yake ya taifa ya England itakayokwenda kushiriki mikikimikiki ya Euro 2024 huko Ujerumani. Mourinho alisema England ina nafasi ya kushinda taji hilo la ubingwa wa Ulaya, sambamba na Ureno, ambayo ni nchi yake.