Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eric Cantona kipaji cha soka safi na domo chafu

Eric Cantona Mkali Eric Cantona

Wed, 3 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Eric Cantona, amerusha jiwe kwa nchi yake akiliponda soka la nchi hiyo kwamba halina mvuto kwa kukosa mashabiki.

Cantona amesema soka la Ufaransa halina historia wala mashabiki kwani huwezi kukuta mji mmoja una timu angalau mbili.

Akifafanua zaidi Cantona amesema Ufaransa hakuna mashabiki wa mpira wa kutosha kushangilia timu zaidi ya moja katika mji mmoja...hii ni kwa sababu nchi hiyo haina historia ya soka.

Maneno haya yanaweza kuwa na ukweli lakini hali kama hiyo ipo kwa nchi nyingi sana duniani, siyo Ufaransa tu.

Labda kwa kuwa yeye ni Mfaransa hivyo anaisemea nchi yake, lakini historia ya Cantona na Ufaransa inaweza kutoa picha nyingine kabisa.

Cantona tangu anacheza soka alikuwa na migogoro na nchi yake kiasi cha kustaafu kuichezea timu ya taifa akiwa bado na umri mdogo sana.

Migogoro yake na soka la nchi yake limemfabya Cantona awe maarufu zaidi England alikocheza kwa muda mfupi kuliko Ufaransa alikozaliwa na kucheza kwa muda mrefu.

MIKASA YA CANTONA

Msimu wa 1991/92 klabu ya Leeds United ilishinda ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza England.

Wakati huo daraja la kwanza ndiyo lilikuwa la juu zaidi, lakini hata hivyo huo ndiyo ulikuwa msimu wa mwisho wa mfumo wa aina hiyo.

Kuanzia msimu wa 1992/93 ligi ndipo ikaanza Ligi Kuu hii tunayoiita EPL ambayo ipo hadi sasa.

Katika kikosi cha ubingwa cha Leeds United kulikuwa na nyota kutoka Ufaransa aliyeitwa Eric Cantona.

Huyu ni mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea kwenye ligi ya England.

Msimu uliofuata akahamia Manchester United ya Alex Ferguson ambayo ilikuwa inajengwa.

Huyu ndiyo mchezaji wa kwanza kulipiwa ada ya uhamisho ya pauni milioni moja.

Kabla ya hapo hakukuwa na mchezaji ndani ya England alivuka ada ya uhamisho ya pauni laki tisa.

Ndani ya Manchester United, Eric Cantona anapewa heshima ya kuwa mmoja wa wachezaji waliojenga msingi wa mafanikio ya Alex Ferguson hadi baadaye kuitwa Sir.

Lakini licha ya uwezo wake mkubwa, Cantona pia alitambulika kama mmoja wa wachezaji wakorofi kuwahi kutokea katika historia ya mchezo huu mzuri.

Alianza kuchezea timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 1987 alipoitwa kwa mara ya kwanza na kocha Henri Michel kwa ajili ya mchezo dhidi ya Ujerumani Magharibi uliofanyika Septemba 1988.

Lakini baadaye kocha akamuacha, kitendo kilichomkera Cantona na kumbwatukia kocha huyo kwenye mahojiano ya moja kwa moja kwenye TV akimuita ‘gunia la mav**’.

Maneno haya yakamponza na kufungiwa kuchezea timu ya taifa kwa mwaka mmoja.

Akabaki anacheza soka la klabu tu na mwaka mmoja baadaye yaani 1989 akiichezea klabu ya Marseille akafanya kituko kingine kabla hajamaliza adhabu ya timu ya taifa.

Ilikuwa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Torpedo Moscow ambapo Cantona alipiga mpira kwa hasira jukwaani kwa mashabiki na kuvua jezi na kuichana akikasirishwa na kitendo cha kutolewa na kocha.

Kosa hili likamfanya afungiwe mwezi mmoja na klabu yake.

Baada ya adhabu hiyo akatolewa kwa mkopo wa miezi sita kwenda klabu ya Bordeaux na ilipoisha akapelekwa kwa mkopo mwingine wa mwaka mmoja klabuni Montpellier.

Akiwa Montpellier Cantona akajikuta tena kwenye wakati mgumu baada ya wachezaji wenzake sita kuitaka klabu kumuondoa mchezaji huyo kufuatia kumpiga na kiatu usoni mchezaji mwenzake Jean-Claude Lemoult baada ya ugomvi baina yao.

Lakini washikaji zake wa karibu klabuni hapo kama Laurent Blanc na Carlos Valderrama ambao baadaye walikuwa wachezaji muhimu kwenye timu ya taifa, wakamuelewa abaki lakini akafungiwa kwa siku kumi kwenda uwanja wa mazoezi.

Licha ya vurugu hizo, Cantona alikuwa mchezaji muhimu uwanjani na kuisaidia Montpellier kushinda Kombe la Ufaransa (sawa na Kombe la Shirikisho la Azam Sports hapa nchini).

Klabu yake ya Marseille ikamrudisha lakini hata hivyo akaingia kwenye migogoro na kocha Raymond Goethals pamoja na mwenyekiti wa klabu, Bernard Tapie.

Akauzwa kwenda klabu ya Nimes na akiwa huko akambabua refa na mpira kwenye moja ya mechi za klabu yake baada ya kukerwa na uamuzi mmojawapo.

Akapelekwa kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka Ufaransa na kufungiwa kwa mwezi mmoja.

Cantona akajibu mapigo kwa kuwafuata wajumbe wa kamati ile, mmoja baada ya mwingine, na kuwatukana akiwaita wapuuzi.

Wajumbe wakaongeza adhabu yake na kuwa miezi miwili.

Cantona akaona wanamtania, alichofanya akaacha mpira wenyewe kabisa na kutangaza kustaafu.

Lakini kocha wa timu ya taifa, Michel Platini, ambaye alikuwa anamkubali sana Cantona , akambembeleza afute uamuzi wa kustaafu na arudi uwanjani.

Cantona akakubali ushauri huo na kufutwa uamuzi wa kustaafu. Kocha mwenye heshima sana Ufaransa wakati huo, Gerard Houllier akamshauri Cantona kutafuta timu England na kuachana na migogoro ya Ufaransa.

Mitcheli Platini akamshawishi kocha wa Liverpool, Graime Souness, kumchukua mchezaji huyo lakini akakataa.

Akapelekwa Sheffield Wednesday lakini klabu hiyo ambayo ndiyo ilitoka kupanda daraja, haikuwa na bajeti ya kumudu mshahara wake...ikajitoa japo alishajiunga nayo mazoezini kwa wiki mbili.

Ndipo akaenda Leeds United na kilichofuata baada ya hapo ni historia.

Chanzo: Mwanaspoti