Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Enock Mayala kama Saido Ntibazonkiza tu!

Sd Enock Mayala Enock Mayala kama Saido Ntibazonkiza tu!

Mon, 16 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Straika wa Polisi Tanzania raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Enock Mayala, juzi alifunga mabao mawili, akiiwezesha timu hiyo kushinda ugenini, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, mabao 2-0 dhidi ya Namungo kwenye mechi ya Ligi Kuu

Tanzania Bara akiingia katika orodha ya wachezaji waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo na kupachika mabao mechi yao ya kwanza tu.

Mayala ameingia kwenye rekodi aliyoiweka kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza, ambaye alicheza mechi ya kwanza akiwa amesajiliwa akitokea Geita Gold katika kipindi hiki cha dirisha dogo lililofungwa jana saa sita usiku, mechi yake ya kwanza tu akifunga mabao matatu 'hat-trick' na kuiwezesha timu yake kushinda mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, alisema pamoja na kumuachia straika Vitalis Mayanga, lakini wamesajili mastraika watatu ambao watakuwa na kazi ya kuiondoa mkiani, ambao ni Kelvin Sabato, Ibrahim Hilika na straika huyo ambaye tayari ameshaanza kufanya vitu vyake.

Kocha Msaidizi wa Polisi Tanzania, John Tamba, alisema ameonyesha kufurahishwa na straika huyo akisema atawasaidia sana kwani tatizo lao lilikuwa ni mtu wa kuweka mpira ndani ya wavu.

"Nimepokea kwa furaha kubwa, tulikuwa na uhaba wa mfungaji tunashukuru, mchezaji huyu tumefanya mazoezi wiki mbili, hakucheza mechi za nyuma kwa sababu hakuwa na vibali, kwa sasa vimekamilika sasa ndiyo ameanza, na bado tuna vita ya kujikwamua mkiani," alisema Tamba.

Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi, alisema lawama zote atupiwe yeye kwa timu yake kukubali kipigo cha mabao 2-0 nyumbani.

"Timu kama haikucheza vizuri, lawama lazima abebe mwalimu, inasikitisha kufungwa na timu ya chini halafu iko pungufu, tumetengeneza nafasi ambazo hatukuweza kuzitumia, safu yangu ya ulinzi haikuwa nzuri, nitatumia muda uliopo kurekebisha hali, lakini mimi ndiyo nabeba lawama kwa hili," alisema kocha huyo.

Polisi Tanzania imefikisha pointi 14 kwa mechi 20 ilizocheza ikiwa nafasi ya 15, huku Namungo ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 26.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live