Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Enock Atta atoa shutuma nzito

Atta Enock Enock Atta atoa shutuma nzito

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Enock Atta Agyei ametoa shutuma nzito kwa waajiri wake hao kuwa tangu alipoumia akiwa nje kwa miezi mitano sasa ametelekezwa, akidai kuwa hajaingiziwa mishahara ya miezi mitatu ambavyo kikanuni ni kama mkataba umevunjiwa.

Mshambuliaji huyo ambaye alijiunga na Singida kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea AC Horoya mwanzoni mwa msimu huu ameliambia Mwanaspoti, amekuwa akijaribu kuwapigia simu viongozi wa timu hiyo kujua sababu ya wao kutokumjali licha ya kuumia akiwa ndani ya timu yao wamekuwa hawapokei wala kujibu jumbe zake.

“Nimekuwa majeruhi kwa muda wa miezi mitano sasa timu hainijali nipo tu nyumbani na jitihada zangu za kupiga simu na kutuma meseji hazinisaidii kwani sijibiwi na hata simu ikipokewa wamekuwa wakiishia kunidanganya hakuna wanachokifanya kwaajili yangu,” alisema Enock Atta na kuongeza;

“Bado nina mkataba wa miaka miwili na nusu sasa walimpigia simu wakala wangu kuwa wanataka kuachana na mimi kwasababu sina ninachokifanya ndani ya timu ilihali niliumia nikiwa kikosini na hawanijali.”

Alisema baada ya uamuzi wao huo alikubaliana na wakala wake kuwa yupo tayari kuachwa lakini wanatakiwa kumlipa fedha zake za mkataba uliobaki lakini haoni hilo likifanyika na anashangazwa na suala la kuto kuingiziwa mshahara ilihali yeye bado ni mchezaji wao na wengine wameingiziwa.

“Baada ya kuwa nje ya timu kuanzia mwanzo wa msimu ambapo walikuwa wananikata dola 500 huku wakiwa na taarifa ya mimi kuumia hii ilikuwa inakatwa kwa madai kuwa timu haifanyi vizuri na hicho kipengele kwenye mkataba wangu hakipo,” alisema mchezaji huyo na kuongeza;

“Ni miezi mitatu sasa sijapata mshahara wangu huku kukiwa na taarifa za wachezaji wenzangu wote kulipwa nimewatafuta viongozi hawapokei simu wala hawajibu meseji nipo tayari kuvunjiwa mkataba nirudi kwetu kwasababu sina ninachokifanya huku.”

Alisema kuanzia Julai hadi Oktoba wamemuingizia mshahara kama kawaida ambao ni Dola 500 kwa mwezi lakini baada ya hapo hajapokea mshahara wake na hafahamu shida ni nini huku akikiri kuwa amevumilia vya kutosha sasa ameamua kuzungumza baada ya kuona hali haielewi anawadai mwezi Juni, Novemba na Desemba.

Alipotafutwa kiongozi wa timu hiyo simu yake iliita bila kupokewa ndipo gazeti hili lilipoamua kumtafuta msemaji wa timu hiyo Hussein Massanza ambaye alikiri kuwa mchezaji wao huyo ni majeruhi na yuko nje ya timu kwa ajili ya kujiuguza lakini akaeleza kuwa madai yake ya malipo hayafahamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live