Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

England yamwaga pesa kuajiri walinzi Qatar

England World Cup.jpeg England yamwaga pesa kuajiri walinzi Qatar

Tue, 1 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia timu ya taifa ya England inaonekana kujipanga vilivyo ili kuhakikisha wachezaji na viongozi wake wanaishi vizuri katika kipindi chote watakachokuwa Qatar kwa ajili ya michuano hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun ni kwamba wake na wachumba wa wachezaji wa England watakuwa chini ya uangalizi mkali wa walinzi ambao baadhi yao watakuwa wanalipwa na wachezaji na wengine watapokea mishahara kutoka Chama cha Soka England kwa ajili ya kazi hiyo.

Inaelezwa kuwa walinzi hao watakuwa na kazi ya kuzilinda familia za wachezaji zisije kufanyiwa uporaji au kukiuka sheria kali za nchi hiyo.

“Kumbuka wachumba na wake wa wachezaji wengi watakuwa Qatar. Wataenda na vito na mavazi ya thamani na hiyo inaweza kuwa sababu ya wao kuwindwa sana ili wasiporwe,” zilisema taarifa za ndani.

Kwa taarifa ambazo hazijathibitishwa na Chama cha Soka England ni kwamba gharama za kuwalipa walinzi maalumu kwa ajili ya familia za wachezaji wao hadi michuano itakapomalizika zinaweza kufikia Euro 150,000 (Sh300 milioni).

Walinzi hao baadhi watasafiri kutoka nchini England na wengine watakuwa wale wa kampuni za ulinzi ambayo yapo nchini Qatar.

Chama cha Soka England kinaamini kuwalipa walinzi kwa ajili ya kuzilinda familia za wachezaji itafanya timu ifanye vizuri kwani mastaa wao watakuwa na amani ya mioyo kuwa familia zao zipo salama, hivyo hata watakapokuwa uwanjani akili zao watakuwa wanazielekeza katika mechi na si vinginevyo.

Mwezi uliopita ilitoka taarifa kwamba wake wa wachezaji wamekodi boti yenye thamani ya Euro 1 bilioni watakayokuwa wanaitumia kula bata katika fukwe za Qatar.

Boti hiyo ina mabwawa sita ya kuogelea, saluni, migahawa na baa. Katika meli hiyo wake wa wachezaji watakuwa na uhuru wa kunywa pombe bila ya kujificha kwani ni moja kati ya maeneo ambayo yameruhusiwa na waandaaji wa mashindano.

Kwa mujibu wa sheria za Qatar hairuhusiwi mtu kunywa pombe hadharani, lakini kuelekea katika mashindano hayo yamechaguliwa maeneo maalumu kwa ajili ya burudani za aina hiyo.

Meli hiyo inaweza kuhudumia hadi wageni 6,762 na malipo yake kwa siku yanaanzia Euro 300 kwa mtu mmoja na kwa chumba chenye vitanda viwili hufikia hadi Euro 690.

Wakati siku zinazidi kukatika kabla ya mashindano hayo, malazi bado yanaonekana kuwa ni changamoto kubwa nchini humo na watu wengi watalazimika kuishi kwenye sehemu mbadala badala ya hoteli kwa sababu ni chache.

Qatar imeamua kukodi meli kubwa zenye uwezo wa kuwalaza watu zaidi ya 10,000, pia imemalizia ujenzi wa vyumba vilivyojengwa ndani ya makontena ambapo watu watakuwa wakiishi humo mpaka mashindano yatakapomalizika.

Makontena hayo ndani yake yamejengwa vyumba na kuwekwa vitanda vyenye hadhi ambapo ikiwa shabiki atataka kulala kwa siku moja itamlazimu kulipa kiasi kisichopungua Pauni 200 kwa usiku.

Makontena hayo yameongeza jumla ya vyumba 30,000 zikiwa zimebaki takriban siku 21 kabla ya mashindano hayo kuanza. Qatar inatarajiwa kuwa nchi ya kwanza kwa mashindano hayo kufanyika Uarabuni.

Chanzo: Mwanaspoti