Mambo ni moto. England itakuwa na kazi ya kusahau jinamizi la Euro 2020 kwa kurusha kete yake ya kwanza kwenye Euro 2024 leo Jumapili kwa kukabiliana na timu ngumu ya Serbia kwenye mchezo wa Kundi C utakaofanyika uwanjani Veltins-Arena.
Si England wala Serbia iliyowahi kushinda taji hilo la Henri Delaunay Trophy tangu lilipoanzishwa na kushindaniwa na mataifa ya Ulaya, huku timu nyingine kwenye kundi hilo ni Denmark na Slovenia.
Kocha wa Serbia, Dragan Stojkovic, anatajwa kama mmoja wa makocha wenye vipaji vya hali ya juu kitu ambacho kinaaminika anaweza kuwapa wakati mgumu Three Lions kwenye mchezo huo, na wamekwenda Ujerumani wakiwa na matumaini ya kubeba taji hilo la Ulaya.
Kwenye kikosi hicho cha Serbia kuna mastaa matata kabisa kama straika wa Juventus, Dusan Vlahovic, mkali wa Ajax, Dusan Tadic na kiungo wa Al-Hilal, Sergej Milinkovic-Savic pamoja na fowadi Aleksandar Mitrovic, wanaweza kuleta matatizo makubwa kwenye kikosi cha England.
England inayonolewa na Gareth Southgate inaamini huu ni wakati wao wa kufanya kweli kwenye fainali hizo, wakiamini wamekwenda na wachezaji wa maana kabisa, akiwamo straika Harry Kane na kiungo Jude Bellingham. Wakati wengine matata kabisa kwenye kikosi cha England ni Bukayo Saka na Phil Foden pamoja na Trent Alexander-Arnold waliobeba matumaini makubwa.
Mechi nyingine za mikikimikiki hiyo ya Euro 2024 zitakazopigwa leo, Poland itakuwa na kibarua kizito cha kuikabili Uholanzi katika mechi ya kibabe kabisa, huku Slovenia itakuwa na kasheshe zito mbele ya Denmark.