Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eng. Hersi apewe maua yake

Hersiiiii Eng. Hersi apewe maua yake

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, anafanya kazi kubwa sana ya kuijenga klabu hiyo uwanjani.

Hersi kijana msomi mwenye mawazo ya kimapinduzi, amekuwa mbunifu kwenye kuhakikisha kila uchao Yanga inakuwa mbele ya wengine kimafanikio.

Tangu aingie madarakani kama Rais wa Klabu Julai mwaka 2022, Hersi ameibadilisha Yanga na kuwa imara sana uwanjani kwa kufanya sajili bora na kuimarisha benchi la ufundi.

Lakini hiyo kama haitoshi, yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anajenga uhusiano wa kitaasisi baina ya Yanga na klabu na taasisi zingine za kimichezo.

UHUSIANO NA TFF

Kabla Hersi hajaingia madarakani, Yanga ilikuwa na uhusiano mbaya sana na TFF.

Mara kadhaa taasisi hizi mbili kubwa zaidi za soka hapa nchini zilikuwa zikilumbana kwa mambo madogo madogo tu na kuleta taharuki kubwa.

Rejea kauli ya Mohamed Mchengerwa alipokuwa waziri wa michezo wa wakati ule mechi ya Yanga na Simba inashindwa kufanyika kutokana na kubadilishwa muda wa kuanza mchezo. Alisema TFF na Yanga kaeni chini malizeni tofauti zenu.

Yanga na TFF walikuwa na tofauti nyingi sana za kimtazamo ambazo msingi wake hasa ulikuwa udhaifu wa Yanga uwanjani.

Kutokana na kukosa timu imara huku wapinzani wao Simba wakiwa bora, Yanga waliishia kuilaumu TFF kwa kila kilichowakuta. Hapo ndipo msemo wa “Wallace Karia ni Simba” ulitawala midomo ya mashabiki wa Yanga.

Lakini alipoingia madarakani Hersi, akaondoa hilo. Amejenga uhusiano mzuri na TFF na sasa Yanga na shirikisho hilo wanaongea lugha moja.

Hata mashabiki wa Yanga hawaseni tena kwamba Karia ni Simba.

Hii inatokana na mafanikio yao ya uwanjani ambayo pia huwezi kuyatenganisha na Hersi lakini pia sera nzuri za kijana huyo wa kimjini kuelekea kutengeneza taswira nzuri ya klabu yake.

UHUSIANO WA KIMATAIFA

Wakati wa uzinduzi wa African Football League, Hersi alikuwa mstari wa mbele kuonana na viongozi wakubwa wa mpira duniani, Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa CAF, Patrice Motsepe.

Alihakikisha wanatoka hapa nchini wakiwa na mawasiliano naye kiasi kwamba akiwatafuta wakati wowote anawapata. Hilo limedhihirika mwishoni mwa wiki iliyopita pale Hersi alipoenda Afrika Kusini.

Kwanza alipata fursa ya kutembelea klabu kubwa kuliko zote nchini humo, Kaizer Chiefs. Akakutana na mwanzilishi wa klabu hiyo, Kaizer Motaung, na viongozi wengine wa klabu hiyo.

Akahudhuria mechi ya Soweto Derby kati ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.

Kisha akaonana na viongozi wa FIFA na CAF, Infantino na Motsepe kama alivyokutana nao Dar es Salaam.

Kuonyesha kwamba kukutana kwao Dar es Salaam kulitengeneza uhusiano endelevu, Rais wa FIFA akamuuliza Hersi kuhusu matokeo ya mechi ya WATANI WA JADI.

Hersi bila hiyana akafungua kiganja cha mkono wake na kuonyesha TANO huku akikazia kwa ulimi wake, WE WON FIVE.

Hii ilikuwa na maana kwamba Infantino na Motsepe waliongea kitu fulani na Hersi walipokuwa hapa nchini hasa kuelekea mechi ya Derby ambayo ilikuwa ifanyike wiki takribani mbili baadaye. Kwa hiyo hapa alikuwa anaulizia hilo... kirafiki.

UHUSIANO NA WATU WA MPIRA

Wote mtakumbuka kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi mwaka huu pale kocha mwenye mafanikio zaidi kutoka ukanda wa Kusini mwa Afrika, Pitso Mosimane, alipokuwa mgeni wa Yanga.

Pale Hersi alicheza karata dume kwenye kujenga uhusiano kati ya klabu yake na watu binafsi wenye ushawishi mkubwa kwenye mpira.

Leo hii ni rahisi kwa Yanga kupata ushauri wa kiufundi kutoka kwa kocha huyo mwenye Leseni ya CAF Pro License. Haya yote hayajaja kwa bahati mbaya. Ni mipango ya kisomi kutoka kwa Mhandisi Hersi Said. Apewe maua yake sasa... tusisubiri afe!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: