Rais wa Young Africans SC na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vilabu Afrika, Eng. Hersi Ally Said, leo amefanya mkutano na Chama cha Waandishi wa Habari za Soka Afrika Kusini (South African Football Journalists Association – SAFJA) Sandton, Johannesburg.
Eng. Hersi amekishukuru Chama cha Waandishi wa Habari za Soka Afrika Kusini kwa kuandaa kwa kuandaa mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuitangaza zaidi klabu ya Young Africans.
Mbali na hilo, pia Eng. Hersi amemshukuru Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe kwa kuanzisha Shirikisho la Vilabu Afrika (ACA).
“Shukrani sana Mwenyekiti wa Umoja wa Wandishi hapa Afrika Kusini kwa kuandaa Mkutano huu. Hii ni Fursa nzuri kwenu kupata majibu ya maswali yote mnayotamani kuyajua kuhusu Klabu yetu ya Yanga na Shirikisho la Vilabu Barani Afrika [ACA] ambalo mimi ndio Mwenyekiti wake. Karibuni sana.
“Februari 11, mwaka huu, Yanga ilitimiza miaka 89 tangu kuanzishwa kwake. Ni Klabu kongwe zaidi ya mpira wa miguu Tanzania na ilishiriki kwenye harakati za Uhuru wa Taifa letu. Ni timu ya Wananchi inayogusa maisha ya kila Mtanzania anayependa mpira.
“Yanga ni Timu yenye mafanikio zaidi Tanzania. Ni Mabingwa mara 29 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, anayefatia amebeba Ubingwa mara 22. Msimu huu mpaka sasa tunaongoza Ligi na Inshaallah tutapambana kuongeza Taji la 30 kwenye Kabati letu la Makombe.
“Nimshukuru sana Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika, Patrice Motsepe kwa kuanzisha Shirikisho la Vilabu Afrika. Wazo lake ni kupata sauti ya Vilabu ndani ya CAF.
“Mpira unachezwa na wachezaji na wote wanatoka kwenye Vilabu. Kuwa na Shirikisho la Vilabu inasaidia kufikisha moja kwa moja changamoto zake na kuona jinsi gani mnaweza kusaidia maendeleo ya Vilabu kwa haraka,” alisema Eng. Hersi.