Kiungo Mshambuliaji wa Dodoma Jiji FC, Emmanuel Martin amesema ataendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao, huku akidai msimu uliopita ulikuwa mgumu kwake.
Martin, mchezaji wa zamani wa Young Africans na JKT Ruvu anayeweza kucheza kama Kiungo Mshambualiji ama Beki wa Kushoto, ana mkataba wa miwili na Dodoma Jiji FC unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao.
Msimu uliopita katika nafasi ya Beki wa Kushoto, kocha Melis Medo alikuwa akiwaanzisha Adeyum Saleh ama Abubakari Ngalema na katika nafasi ya winga Rashid Chambo ama Mwana Kibuta.
Beki huyo ambaye ni Nahodha Msaidizi katika kikosi hicho, amesema msimu uliopita ulikuwa mgumu kwake kutokana na ushindani wa namba uliokuwepo kutoka kwa Adeyum na Ngalema.
“Ulikuwa msimu mgumu mno kwangu kuliko msimu yote niliyowahi kucheza ligi, ugumu umekuja kutokana na ubora wa wachezaji walioongezwa na katika soka hilo ni jambo la kawaida.
“Changamoto ndiyo inakukomaza, inakufanya uzidi kuwa bora, najipanga msimu ujao mambo yatakuwa mazuri zaidi, nitapambana kuhakikisha narudisha namba yangu,sasa hivi nimepona na nipo vizuri,” alisema beki huyo, ambaye amewahi kuichezea JKU ya Zanzibar.
Matarajio yake ni timu hiyo kufanya vizuri zaidi msimu ujao zaidi ya msimu uliopita, kwani wachezaji watakuwa wamezoeana zaidi.
“Mzunguko wa pili tulicheza vizuri, ila mzunguko kwa kwanza haukuwa mzuri kutokana na ugeni wa baadhi ya wachezaji,” amesema beki huyo.