Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

El Capitano wenye vitambaa vyao Ligi Kuu

Bkari Mwamnyeto Nondo El Capitano wenye vitambaa vyao Ligi Kuu

Sun, 3 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha ni kiongozi wa wachezaji na huchaguliwa na wenzake kwa kura au kuteuliwa na kocha.

Jukumu lake kubwa ni kuongoza wenzake ndani na nje ya uwanja katika mambo mbalimbali yanayowahusu wachezaji, hivyo huheshimiwa na wenzake.

Vigezo ambavyo mara nyingi hutumika kumchagua au kumteua ni pamoja na uzoefu na kukaa muda mrefu katika timu, mwenye ushawishi na uwezo wa kuongoza wenzake.

Pia kutokana na mwenendo wake, anaweza akavuliwa unahodha au matakwa ya benchi la ufundi na viongozi.

Kila timu ina nahodha na kwenye Ligi Kuu Bara yenye timu 16 wamo. Wapo walioendelea kuwa manahodha walioupata msimu uliopita na baadhi ya timu zimebadili wa kushika cheo hicho.

Hapa, Mwanaspoti linakuletea manahodha wote 16 wa kila timu Ligi Kuu Bara msimu huu.

SIMBA - BOCCO

Mshambuliaji John Bocco ndiye nahodha wa Simba ikiwa ni mwaka wa sita sasa akiwaongoza Wekundu wa Msimbazi hao.

Bocco alikabidhiwa rasmi kitambaa hicho Januari 2018, baada ya aliyekuwa nahodha wa Simba kwa wakati huo, Mzimbabwe Method Mwanjali kuachwa dirisha dogo la msimu wa 2017/2018.

Wasaidizi wa Bocco ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe.

YANGA - MWAMNYETO

Beki wa kati, Bakari Mwamnyeto ndiye nahodha wa mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu.

Mwamnyeto alikabidhiwa usinga wa Yanga rasmi Septemba 2021 baada ya kuondoka kwa Mghana Lamine Moro aliyekuwa nahodha mkuu huku Mwamnyeto akiwa msaidizi wake.

Msadizi wa Mwamnyeto ni beki wa kati mwenzake, Dickson Job akisalia baada ya kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kusepa zake Azam FC.

AZAM FC - BAJANA

Kiungo wa kati Sospeter Bajana ndiye nahodha mkuu wa matajiri wa Ligi Kuu, Azam FC kwa msimu huu.

Bajana alianza kutumikia cheo hicho mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuondoka kikosini hapo kwa aliyekuwa nahodha mkuu Aggrey Morris na msaidizi wake Bruce Kangwa.

Idriss Mbombo, Daniel Amoah, wamekuwa pia wakivaa kitambaa hicho pale anapokosekana Bajana uwanjani.

SINGIDA - ONYANGO

Beki wa zamani wa Simba, Mkenya Joash Onyango ndiye nahodha mkuu wa Singida Big Stars kwa sasa.

Onyango amechukua kitambaa hicho kutoka kwa Pascal Wawa aliyechwa kikosini hapo, pia aliwahi kucheza Simba na Azam.

Wasaidizi wa Onyango ni Gadiel Michael na Bruno Gomes.

MASHUJAA - MAKAPU

Klabu mpya kwenye Ligi Kuu, Mashujaa kutoka kigoma nahodha wake ni staa wa zamani wa Yanga na Ihefu, Said Juma ‘Makapu’.

Beki huyo anayemudu pia kucheza eneo la kiungo ndiye amekabidhiwa usinga kutokana na uzoefu wake kwenye ligi.

Wasaidizi wa Makapu hawajafahamika kwani timu ndio kwanza imepanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Championship.

JKT - KATANGA

Wafunga buti hawa nao wamerejea tena Ligi Kuu baada ya kuikosa kwa misimu miwili mfululizo, anayevaa kitambaa cha unahodha ni beki Edson Katanga, akisaidiwa na mshambuliaji Edward Songo ambao wapo kwenye timu hiyo kwa misimu kadhaa sasa.

IHEFU - MAHUNDI

Walima mchele hawa wa Mbarali, Mbeya wameendelea kukomaa na nahodha wa msimu uliopita Joseph Mahundi aliyechukua usinga kutoka kwa Joseph Kinyozi aliyeachwa.

Msaidizi wa Mahundi ni kiungo wa zamani wa Yanga, Raphael Daud Loth.

DODOMA - NSATA

Walima Zabibu hawa wa Dodoma msimu huu wameendelea na nahodha wao Augustino Nsata anayecheza eneo la beki wa kati.

Staa wa zamani wa Yanga, Emmanuel Martin na kiungo Salmin Hoza ndio wasaidizi wa Nsata pale Dodoma.

KMC - AWESU

Kocha mkuu mpya wa KMC, Abdihimid Moallin alipofika kikosini hapo alimteua kiungo Awesu Awesu kuwa nahodha mkuu.

Awesu anachukua nafasi ya Mrundi Emmanuel Mvuyekure aliyetimkia Rayon Sports ya Rwanda huku msaidizi wake akiwa Sadala Lipangile.

COASTAL - AJIBU

STAA wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars, Ibrahim Ajibu ndiye nahodha mpya wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’.

Ajibu amekabidhiwa kitambaa cha unahodha na kocha mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera, ambaye pia kama Ajibu, wote ni wapya kikosini hapo.

Kabla ya Ajibu, kitambaa hicho kilikuwa kikivaliwa na Mtenja Albano aliyetimkia Dodoma Jiji.

NAMUNGO - DOMAYO

Kiungo wa zamani wa Yanga na Azam, Frank Domayo ndiye nahodha mpya wa Wauaji wa Kusini, Namungo.

Domayo amekabidhiwa kitambaa cha unahodha kutoka kwa Hamis Mgunya huku msaidizi wake akiwa kiraka wa zamani wa Simba, Erasto Nyoni.

MTIBWA - MAKAKA

Kipa wa Mtibwa Sugar, Mohamed Makaka ndiye nahodha mpya wa kikosi hicho cha walima miwa wa Turiani, Morogoro.

Makaka anachukua jukumu hilo ambalo kwa msimu uliopita lilikuwa chini ya beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyetimkia Ihefu.

PRISONS - ASUKILE

Mlimisi Asukile? Basi mtaendelea kumuona kwenye Ligi Kuu akiwa ndani ya jezi za Wajelajela, Tanzania Prisons.

Asukile ambaye ni kiraka, ndiye nahodha mkuu wa maafande hao huku akisaidiwa na beki Jumanne Elfadhili.

KAGERA - LUHENDE

Wakata miwa hawa wa Bukoba kitambaa chao cha unahodha kwa msimu huu kitaendelea kuwa kwenye mkono wa kushoto wa beki David Charles Luhende.

Luhende aliyedumu Kagera kwa muda mrefu atakuwa akisaidiwa jukumu la unahodha na Abdallah Seseme.

KITAYOSCE - KOMANJE

Wakali hawa kutoka Tabora walipanda Ligi Kuu msimu huu na kuanza kwa kichapo cha mabao 4-0, huku mechi ikishindwa kumalizika kutokana na kuwa pungufu uwanjani baada ya mastaa wake wengi kutokuwa na vibali, nahodha wao ni Komanje Sandale.

Komanje anacheza eneo la beki ya kati, aliiongoza Kitayosce kupanda Ligi Kuu kutoka Ligi ya Championship.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: