Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eeh! Straika Simba apoteza dole gumba

Adam Salamba Mk Adam Salamba

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Unamkumbuka Adam Salamba? Straika huyo wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga Libyan Stadium FC ya Libya, kumbe aliwahi kupoteza dole gumba la mguu wa kulia!

Unaweza kudhani utani, lakini nyota huyo aliyewahi kutamba na Stand United, Lipuli FC na Namungo anasimulia mkasa wake alipozungumza na Mwanaspoti kwa kusema tukio hilo hadi leo limebaki kichwani mwake.

Salamba aliyecheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa zikiwamo za Al Jahra ya Kuwait, JS Saoura ya Algeria na El Mahalla ya Misri, amesema amewahi kukutana na changamoto tofauti kwenye majukumu ya uchezaji, lakini kubwa ni lile la kujikuta hana kidole gumba cha mguuni katika namna ya ajabu kabisa.

Salamba amesema tukio lilitokea wakati alipokodishwa kwa ajili ya mechi za ndondo na kumfanya aendelee kumshukuru Mungu kwa uwezo alionao usio na mfano.

"Nakumbuka siku moja nilikodiwa kwenda kucheza mechi ya ndondo kwa Sh30,000 sikumbuki ilikuwa ni mwaka gani, ila ilikuwa mkoani Geita eneo la Kome, baada ya kufika uwanjani, nikavaa njumu tayari kwa kazi uwanjiani," amesema Salamba na kuongeza;

"Lakini wakati nashika vidole vya miguu nilishangaa kwani sikuona kidole gumba cha mguu wa kulia, japo vidole vingine vyote vilikuwepo. Hali hii ilinishtua na kuamua kuvua kiatu, ajabu kilikuwapo kama kawaida, ila nikivaa tu kinapotea na nilifanya hivyo zaidi ya mara tano, kila nikishika kidole gumba nilikuwa sikioni."

Salamba mwenye umri wa miaka 24, amesema aliamua kufanya maamuzi ya kuokoa maisha yake kwa kurudisha fedha alizopewa na kusepa zake.

"Niliwarudishia pesa zao na kuchukua begi langu, kisha nikaondoka uwanjani, nikiwaacha timu pinzani wakishangilia tukio hilo. Naomba mniwe radhi siwezi kutaja timu hizo, lakini ni tukio lililobaki kichwani hadi leo," amesema Salamba aliyeifungia Simba mabao manne katika Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 iliyomsdajili akitokea Lipuli ambapo alitoka kuifungia mabao manane.

"Ilikuwa siku mbaya sana kwangu, maana hiyo pesa ilikuwa kwenye mahesabu makali, nilipanga kumpa mama Sh20,000 na Sh10,000 ni kula msosi wa nguvu na matumizi madogo, lakini kila kitu kilibadilika," amesema nyota huyo aliyeanza kucheza soka mtaani tangu akiwa na miaka 10 akiwa na ndoto za kuja kuwa staa mkubwa kabla ya Stand United kumtambulisha kwenye ligi mwaka 2016.

Chanzo: Mwanaspoti