Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eeh! Dube alianzisha Azam FC

Dube Awataja Simba Baada Ya Ushindi Wao Wa 5 0 Prince Dube

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Azam FC jana ilipata ushindi wa 12 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku ikimkosa straika wake hatari, Prince Dube ikiwa ni mechi ya pili mfululizo, ikielezwa ni majeruhi lakini yameibuka mapya baada ya kubainika kuna jambo linaendelea baina ya nyota huyo Mzimbabwe dhidi ya mabosi wa klabu hiyo.

Dube mwenye mabao saba hadi sasa katika Ligi Kuu, amekosekana kwenye mechi mbili zilizopita za ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na Singida Fountain Gate kwa kilichoelezwa ni majeruhi, japo imebainika hana tatizo lolote isipokuwa yupo kwenye mgomo baridi.

Taarifa ambazo zimenaswa na Mwanaspoti ni Dube ameanzisha mgomo huo baridi baada ya kubaini kuna ofa kibao zimekuja Azam ili kuhitajiwa kwenda kuzitumikia klabu hizo, lakini zimekuwa zikikaushiwa ndio maana sasa anashinikizwa alainishiwe wakati mkataba wake ukielekea ukingoni.

Dube hajaonekana kwenye mechi mbili za Azam zilizopita kuanzia ule mchezo wa Prisons kule Mbeya ilipotoka sare ya bao 1-1, pia jana wakati kikosi chao kikishinda ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate kwa bao 1-0.

Mapema taarifa ya Azam ilisema mshambuliaji huyo ni majeruhi, ingawa alionekana yuko sawa Uwanja wa Benjamin Mkapa akiishuhudia Yanga ikicheza dhidi ya CR Belouizdad wikiendi iliyopita huku aligoma kuongea wala kupigwa picha.

Hata hivyo, imefahamika Dube hayupo kwenye maelewano mazuri na uongozi wa klabu yake kutokana na uwepo kwa ofa mbalimbali ambazo wamekuwa wakizigomea kumuuza.

Mmoja wa wasimamizi wa mshambuliaji huyo, amesema Dube hakuwa anajua juu ya ofa hizo, ingawa baadaye alikuja kujulishwa kwa siri na watu wa hizo klabu ambazo zimekuwa zikimtaka.

"Unajua ofa zikija ni kwa klabu kwa kuwa Prince (Dube) bado yuko kwenye mkataba na Azam, lakini na kuhakikishia Azam walikuwa wanazipokea hizi ofa zote, lakini walikuwa hawamjulishi mchezaji kitu ambacho hakukifurahia," amesema wakala huyo jina limehifadhiwa na kuongeza;

"Nadhani wanatakiwa kukaa na kuzungumza naye, mchezaji yeyote anayecheza soka kwa malengo akisikia kitu cha namna hiyo hatafurahia na hiki ndicho kinachotokea kwa Prince."

Mwanaspoti lilijaribu kuwasaka viongozi wa Azam ili kupata ufafanuzi juu ya sakata hilo, lakini simu hazikupokelewa kama ilivyokuwa kwa Dube mwenyewe aliyepigiwa mara kadhaa ili kueleza ukweli wa madai hayo.

Dube alisajiliwa na Azam msimu wa 2020-2021 akitokea The Highlanders ya Zimbabwe na amekuwa mshambuliaji muhimu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwani msimu wa kwanza tu aliifungia mabao 14 katika Ligi Kuu kabla ya kuumia na kukaa hadi aliporejea msimu uliopita alipoifungia mabao 11 na msimu huu ametupia saba.

Chanzo: Mwanaspoti