Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Edu, amekiri kwamba anaelewa kwa nini mashabiki wanaitaka timu kusajili Mshambuliaji katika dirisha la usajili la majira ya joto, lakini ametoa maoni machache kuhusu mipango halisi ya klabu hiyo.
Gabriel Jesus alisajiliwa kwa Pauni Milioni 45 mwaka 2022, lakini ametumia muda mwingi kuwa majeruhi tangu wakati huo, na pia kukiri kwamba hana uwezo mkubwa sana wa kufunga mabao.
Eddie Nketiah ndiye mshambuliaji mwingine pekee wa kati kikosini, lakini hajaanza mara kwa mara tangu Novemba mwaka jana.
Badala yake, Kocha Mikel Arteta amependelea kutumia mawinga waliobadilishwa au washambuliaji wa kati katika nafasi ya ‘namba tisa’ kama vile Leandro Trossard na Kai Havertz.
“Ninaelewa mashabiki wanachoomba, lakini tayari tuna mawazo yetu na shabaha zetu. Tunapanga mengi kabla ya yale tutakayokabiliana nayo,” amesema Edu akiiambia TNT Sports.
“Nitakuwa na wasiwasi ikiwa hatufungi mabao mengi, ikiwa hatutengenezi nafasi, ambayo ni kinyume, nadhani tunaten-geneza sana, tunafunga mabao mengi. Mpango ni kwa kila mwaka kujaribu kuwa bora, nadhani tuko katika wakati mzuri na tuone kama tunaweza kuendelea kuboresha,”
Mabao ya Arsenal ya msimu uliopita yalikuwa shirikishi kupitia kwa Bukayo Saka, Martin Odegaard na Gabriel Martinelli wote wakisajili 15 katika mashindano yote.
Saka ana mabao 16 hadi sasa msimu huu wa 2023/24, lakini hakuna mchezaji aliyevuka mabao 20 kwa msimu mmoja tangu Pierre-Emerick Aubameyang afunge 29 msimu wa 2019/20.
Inaelezwa kuwa Arsenal inamfuatilia mshambuliaji wa Uholanzi wa chini ya miaka 21 wa Bologna, Joshua Zirkzee, kama vile Manchester United.
Nia pia imeoneshwa kwa Dusan Vlahovic, wakati mazungumzo yalifanyika na wawakilishi wa Ivan Toney, lakini walikutana na bei mbaya kutoka kwa Brentford.