“Wachezaji wetu wengi wana vipaji sawa na hawa wachezaji wa Afrika ambao wanatamba Ulaya. Tofauti pekee baina yao na sisi ni ujeuri chanya ambao unakwenda kutengeneza uthubutu. Basi. Hakuna maajabu mengine makubwa ambayo wanayo halafu sisi hatuna.
“Nimemtazama sana Nova. Ni msela. Ni msela ambaye ana sura nzuri ya kiume inayovutia, lakini anacheza soka la shoka, ana kipaji, mshindani kutoka moyoni. Sisi tunatengeneza wachezaji wengi ambao wana vipaji lakini sio washindani kutoka moyoni.
Tunatengeneza vipaji vipi legelege ndani na nje ya uwanja. Nova, kama ilivyo kwa Samatta au Simon Msuva sio kwamba wao ni vipaji vya ajabu ambavyo taifa letu limewahi kuvitoa. Hapana. Ila ni wachezaji washindani ambao tumewahi kuwa nao. Ushindani sio ndani ya uwanja tu bali pia nje ya uwanja. Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kufanikisha mchezaji kufika juu.” - Edo Kumwembe.