Mabosi wa Yanga wamemfuta kazi Kocha Sebastian Nkoma, huku ikielezwa wanasaka kocha mpya wa kuziba nafasi yake licha ya kwa sasa nyota wa zamani wa timu hiyo, Fred Mbuna kushikilia kwa muda na jina la Edna Lema likitajwa kutaka kurudishwa kikosini.
Lema aliyeifundisha timu hiyo kwa muda mrefu tangu ilipopanda daraja kabla ya kuachana nayo Desemba mwaka jana, baada ya kufungwa bao 1-0 na Fountain Gates Princess katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Edna aliyekuwa akifanya kazi akisaidiwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, aliiwezesha Yanga msimu uliopita kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba iliyotetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo na Fountain iliyomaliza ya pili.
Katika moja ya kuonyesha bado anaipenda timu hiyo kocha huyo aliyepo pia kwenye jopo la timu ya taifa aliandika kwenye akaunti zake za mtandao ya kijamii; “Hatuwezi kuwa maadui kwa sababu mimi sio sehemu ya Yanga bado mtabaki kuwa familia yangu, viongozi pamoja na mashabiki niwashukuru tena na tena kwa mapenzi yenu kwangu najua kuna wanaonipenda sana lakini timu kwanza mtu baadaye.”
Tangu Nkoma aliyenyakuliwa kutoka Simba kushika nafasi ya Lema, zipo taarifa kwamba mabosi wa Yanga wanampigia hesabu kumrejesha kikosini.
“Hakuna ukweli juu ya jambo hilo huo ni uvumi tu wa mitandao Yanga bado hawajanitafuta, ila hata ikitokea na kuwa kweli sioni tatizo nitazungumza nao kwa vile mimi ni kocha na wajibu wangu kufundisha,” alisema Lema nyota wa zamani wa Twiga Stars.