Ni mmoja wa makocha wanawake wanaofanya vyema kwenye soka la Tanzania na kuibua baadhi ya nyota wanaotamba ndani na nje ya nchi.
Miaka kadhaa nyuma kabla ya kuondoka Yanga, aliibua vipaji vya Clara Luvanga, Aisha Masaka wanaotamba kwenye ligi za kimataifa Saudi Arabia na England mtawalia.
Mbali na kufanya vyema akiwa na Yanga kabla ya kuondoka msimu wa 2022/23 na kutua Biashara United ya Mara msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara, tayari alishatengeneza jina kubwa kwenye soka la wanawake na kuifanya Yanga tishio licha ya kushindwa kubeba mataji hasa la Ligi Kuu.
Uongozi wa Yanga baada ya kuona mafanikio aliyoyaacha kabla ya kuondoka, umeamua kumrejesha msimu huu na wanaamini atafanya makubwa zaidi ya kurejesha makali ya kikosi hicho.
Mwanaspoti limekuchambulia mambo ambayo atakutana nayo kwenye kuirejesha Yanga kwenye makali na mbio za kuwania taji la kwanza la Ligi Kuu ya Wanawake ikiwamo pia kushiriki michuano ya kimataifa.
KUREJESHA MAKALI
Ndiye kocha mkuu na kazi kubwa ni kuirejesha ile Yanga yenye makali baada ya kutetereka kwa misimu miwili nyuma.
Mbali na kurudisha utawala wa Yanga kwenye soka la wanawake, ana kibarua kingine cha kusaka mataji na aliwahi kuwa kwenye nafasi za juu akiwa na Yanga akiwania mataji.
Pia kocha huyo ana kazi ya kuvipandisha viwango vya nyota wa timu hiyo kama Irene Kisisa 'Rodrigo' ambaye chini yake alikuwa moja ya viungo wenye viwango vya juu katika ligi kabla ya misimu kadhaa haa kushuka.
KUZALISHA KINA MASAKA, LUVANGA WENGINE
Edna ndiye aliyewaibua mastaa wa kike wanaotamba kimataifa akiwamo Masaka anayekipiga Brighton & Hove Albion ya Ligi Kuu ya Wanawake England.
Masaka kabla ya kutimka nchini alikuwa chini ya kocha Edna na aliifungia Yanga mabao 35 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya wanawake kitu ambacho tangu kuondoka kwake hakuna mchezaji mwingine aliyefanya hivyo.
Mbali na Masaka pia Edna aliimfanya Clara Luvanga kuwa bora chini yake kabla ya kutimkia nje ya nchi na anacheza soka la kulipwa Al Nassr ya Saudi Arabia.
Kuondoka kwa Edna kulipunguza ukuaji wa vipaji vya wachezaji ndani ya Yanga hivyo kurejea kwake tunatarajia kuona mastaa wapya wakiibuka.
KUVUNJA UTAWALA WA SIMBA, JKT QUEENS
Kazi nyingine kubwa ambayo inamsubiri ni kuuvunja utawala wa Simba Queens na JKT Queens ambao wenyewe ndio wamekuwa wababe wa timu nyingine katika ligi hiyo.
Wawili hao wenyewe wamekuwa wakizionea timu nyingine kwa kuzifunga wanavyotaka na kupokezana kubeba ndoo ya ubingwa vile wanavyotaka wao, tofauti na timu nyingine.
Kazi hii haitakuwa rahisi kwa sababu wawili hao nao wamekuwa wakijiboresha kila msimu ili waendelee kuwa watawala wa soka la wanawake hapa nchini. Kazi anayo.
KUBEBA UBINGWA WA LIGI
Ni wazi kabisa Edna akishavunja utawala wa Simba na JKT Queens basi atakuwa na nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa ligi hiyo ambao umekuwa ukienda Mbweni na Msimbazi pekee.
Tofauti na Mlandizi Queens ya Pwani hakuna timu nyingine ambayo imewahi kubeba ubingwa huo, hivyo kama Edna atabeba basi ataweka rekodi ya kipekee ya kuwa kocha mwingine ambaye amebeba taji kando na Simba na JKT Queens.
Pia atakuwa ameweka rekodi yake ndani ya Yanga Princess kwa sababu klabu hiyo tangu ipande kucheza ligi kuu haijawahi kuchukua taji hilo zaidi ya kushika nafasi ya pili msimu wa 2021.
KUKATA TIKETI LIGI YA MABINGWA
Kama ilivyo kwenye kubeba ubingwa basi ndiyo ipo hivyo katika kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na hadi sasa Tanzania imewakilishwa na JKT na Simba Queens katika michuano hiyo.
Hili pia ni jambo linalomsubiri kocha huyo katika kibarua chake hicho kwa kuhakikisha Yanga Princess inakuwa timu ya tatu kutoka Tanzania kucheza michuano hiyo mikubwa kwa upande wa klabu.
Hapa kuna kazi ya kufanya zaidi kwa sababu ili wakate tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ni lazima wapambane na mabingwa wengine wa nchi za Afrika Mashariki na bingwa mashindano hayo ya Cecafa ndiye anapata tiketi hiyo.
BATO LAKE NA CHABRUMA LITANOGA
Kama kuna kitu kitamu ambacho kitatokea kwa msimu ujao wa ligi ya wanawake basi ni bato ya kocha Edna na Yanga Princess dhidi ya Ester Chabruma wa JKT Queens kwa kuwa wenyewe ndiye makocha pekee wa kike katika ligi hiyo.
Kando ya kuwa makocha wakike pekee, pia makocha hao wana ujuzi wa kisasa wa kufundisha na hilo wameshalidhirisha katika vikosi vyao tena Chabruma akibeba hadi na ubingwa.
Utamu zaidi ni makocha wote hao wanajuana kwa kuwa walishawahi kucheza pamoja katika timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars', hivyo kila mmoja atakapokutana na mwenzake atataka kumuonesha yeye ni bora zaidi.
UBABE WA DABI YA KARIAKOO
Mabosi wa Yanga kama kuna kitu kinawauma basi ni kuiona timu yao ikiwa ni 'wateja' wa Simba Queens kila wanapokutana katika Kariakoo Dabi. Katika mechi 12 ambazo wamecheza Yanga Princess wamefanikiwa kushinda mechi moja pekee, tena walishinda wakiwa china ya Edna lakini kando ya hapo imekuwa ni vipigo na sare tu.
Simba imeshinda mara nane, wakati Yanga mara moja na sare tatu swali ni Je? Kurudi kwake kutaongeza rekodi ya ushindi au wataendelea kuwa mateja.
Sasa kurejea tena kwa Edna ndani ya Yanga Princess kunaamsha hali ya mabosi wa timu hiyo kuona hawaendelei kupokea vichapo katika dabi hiyo.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumza kurejea kwake ndani ya Yanga Princess, Edna Lema amesema: "Kwanza nashukuru, nimefurahi kurejea tena kwa sababu hapa ndiyo sehemu ambayo nilianza maisha yangu ya ukocha kwa maana ya Klabu ya Yanga.
"Nimerejea tena kwa kipindi kingine nafikiri tunahitaji kutengeneza timu kwa sababu unaweza kuwa na wachezaji wengi lakini hauna timu, kwa hiyo tunataka kuirudisha Yanga Princess ambayo watu wengi walizoea kuiona kwa maana inayocheza vizuri na kupata matokeo mazuri.
"Naamini haitokuwa kazi rahisi lakini kwa sababu ndiyo kazi yetu tunapaswa kufanya hivyo kuhakikisha timu inarejea kwenye uimara wake.
"Naamini tuna nafasi ya kufanya vizuri msimu huu kutokana na aina ya wachezaji tulionao na namna tulivyojipanga, tuna sapoti kubwa kutoka kwa uongozi ambao upo madarakani.
"Cha muhimu ni kuwa na subira kwa sababu mafanikio yoyote ni mchakato na siyo kitu kinachotokea kama ajali, kwa hiyo wawe na subiri, muhimu watusapoti."