Kocha wa zamani wa Yanga Princess, Edna Lema ameingia makubaliano ya mwaka mmoja na klabu ya Biashara United ya Mara kuwa kocha msaidizi kwa msimu wa mwaka 2023/2024 kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi la timu hiyo katika Ligi ya Championship inayoanza Septemba 2, mwaka huu.
Edna amejiunga na timu hiyo leo Agosti 18, 2023 baada ya kusaini mkataba mjini Musoma, Mara ikiwa ni takribani miezi tisa bila kuwa na timu ya kufundisha tangu alipoachana na Yanga Princess Desemba 8, 2022 klabu hiyo ilipovunja mkataba wake pamoja na msaidizi, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na timu kupewa Fredy Mbuna.
Kocha huyo anaungana klabuni hapo na kipa wa zamani wa Taifa Stars, Simba, Yanga na Azam, Ivo Mapunda ambaye pia ametua Biashara United kuwa kocha wa makipa ambapo watakuwa chini ya Kocha Mkuu, Amani Josiah kuiongoza Biashara United kwa msimu huu katika Championship kuhakikisha inarejea Ligi Kuu.
Mjumbe wa bodi ya Biashara United, Agustine Mgendi amesema wamefikia makubaliano na Kocha Edna Lema kuwa kocha msaidizi kwa mkataba wa mwaka mmoja huku ikivutiwa zaidi na uzoefu wake katika kufundisha na kuongoza timu kwa mafanikio ambayo yanaweza kuisaidia klabu yao.
Mgendi amesema kutokana na uzoefu wa kocha huyo wanaamini ataongeza thamani katika mfumo wa klabu yao kwa kushirikiana na benchi zima la ufundi ambalo uongozi umewaamini kuwa watasaidia kuirejesha Ligi kuu.
"Tumemteua kutokana na ubora wa CV (wasifu) yake katika soka sababu ni kocha mzuri atakayeongeza thamani katika benchi la ufundi, na tutaendelea kuboresha kila eneo ambalo linauhitaji na tutafika katika malengo yetu," amesema Mgendi
Mabadiliko hayo makubwa katika benchi la ufundi la Biashara United ni mwendelezo wa mabadiliko ya uendeshaji yanayosimamiwa na Rais wa klabu hiyo, Revocatus Rugumila ambapo tayari wamekamilisha usajili wa wachezaji tisa akiwamo mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Boban Zilintusa, kipa David Kissu, Babilas Chitembe, Caleb John Thomas Malulu, Herbert Lukindo, Paul Ngalema, Salim Sheshe na Godfrey Mapunda.
Akizungumzia mipango na mikakati ya klabu hiyo kuelekea msimu mpya, Rais wa Biashara United, Revocatus Rugumila amesema “Lengo kubwa la klabu ni kuhakikisha timu inarejea Ligi kuu msimu wa 2024/25 na ili kufanikisha hilo ndiyo maana tunafanya usajili wa wachezaji wakubwa kulingana na matakwa ya mwalimu na kuboresha benchi letu la ufundi ili tuwe imara kila idara,"