Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Edna Lema: Sipendi kuzungumza sababu za kuondoka Yanga

Edna Lema Mourinho Edna Lema: Sipendi kuzungumza sababu za kuondoka Yanga

Wed, 6 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Edna Lema sio jina geni kwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini.

Mwanamama huyo ambaye safari yake katika soka ilianza 2001, hivi karibuni alitangazwa kocha msaidizi wa Biashara United baada ya kukaa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa.

Biashara United yenye makao makuu yake mjini Musoma mkoani Mara inakuwa klabu yake ya kwanza ya wanaume kufundisha. Pamoja na mambo mengine anaamini chini ya kocha mkuu Amani Josiah klabu hiyo inayoshiriki Championship itapanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Akisimulia alivyoanza safari katika soka, Edna anasema 2001 alisajiliwa katika timu ya Morogoro Kids kabla ya kuitwa timu ya soka ya taifa ya wanawake 2002.

“Baadaye nilisaini mkataba wa miaka mitatu kwenye timu ya Vijana Queens ya Dar es Salaam hadi 2007 wakati huo pia nikiwa nacheza timu ya taifa. Baada ya hapo nikaacha kucheza soka,” anasema.

Anasema mwaka huohuo wa 2007 baada ya kuacha kucheza mpira alianza kusomea ukocha wa mpira, masomo ambayo alisoma kwa awamu tofauti.

Anasema baada ya kumaliza kozi ya awali alianza kusoma kozi ya kati 2010 ambapo mbali na kusomea ukocha pia alikuwa akijishughulisha na masuala mengine yahusuyo soka ambapo 2014 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Morogoro. “Nilikuwa mwenyekiti kwa miaka minne, mwaka 2015 nikaanza kusoma tena hapo nilisoma na kupata Leseni C,” anasema.

Anaongeza kuwa alijiendeleza kuboresha na kuimarisha ujuzi katika ukocha ambapo 2016 alipata leseni B na mwaka jana akapata leseni A.

Edna anasema kozi za ukocha amesoma katika nchi mbalimbali ikiwamo Ujerumani na Marekani ambako alisomea ukocha wa soka kwa watoto wadogo wa kike na kiume.

Anasema 2016 hadi 2022 ametumikia taifa kama kocha msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya wanawake.

Mbali na timu ya taifa, pia 2019 hadi 2022 alitumika kama kocha mkuu wa timu ya soka ya wanawake ya Yanga Princess ya jijini Dar es salaam.

Hata hivyo, Edna anasema hapendi kuongelea kilichosabanisha akaachana na Yanga Princess kwa maelezo kuwa sio jambo jema kuondoka sehemu kisha ukaanza kuzungumzia mambo ya huko. “Mambo ni mengi wakati mwingine mazingira ya unapokuwa yanaweza yasikupe kile unachotaka au ulichodhamiria ila kikubwa ni kwamba kule tulimalizana vizuri na maisha lazima yaendelee,” anasema.

Kuhusu timu hiyo kutokufanya vizuri kwenye ligi ya wanawake nchini, Edna anasema zipo sababu kadhaa ambazo zikifanyiwa kazi basi timu hiyo itafanya vizuri kama ya kaka zao.

Anasema uzoefu ni moja ya sababu zinazofanya timu hiyo isifanye vizuri na anasema umefika muda wajifunze kwa wenzao kama JKT na Simba ambazo timu zao zina uzoefu katika ligi.

Anasema zipo changamoto kadhaa zinazowafanya wanawake kutokujihusisha na soka nchini lakini anayo furaha kuwa yeye ni miongoni mwa wachache walioamua kujihusisha na mchezo huo hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanawake wengine.

Anasema woga bado ni kikwazo kikubwa kwa wanawake kuamua kufundisha timu za wanaume ilhali hakuna jambo jipya kwani mambo ni yale yale.

Anasema aliamua kuanza kufundisha timu ya wanaume ili kujipa uzoefu zaidi kwani ualimu wa soka unahitaji kujifunza zaidi siku hadi siku.

“Unajua mpira unahitaji uwepo uwanjani kila siku ujifunze kutoka kwa wazoefu zaidi, upate mbinu mpya kila mara kwasbabu ualimu sio kuwa na cheti tu,” anasema.

Anasema katika kila kazi changamoto hazikosekani ila kinachotakiwa ni kuangalia namna ya kupambana nazo ili zisikuondoe kwenye mstari na kwamba ukocha sio kwa wanaume pekee bali hata wanawake wanaweza.

“Wanawake kuna changamoto tumezaliwa nayo na sio kwenye ukocha pekee bali kuna kazi nyingi tunadhani hatuwezi, tunatakiwa kubadilika kwani dunia imebadilika wachukulie mfano Rais wetu Samia Hassan ni mwanamke, hakuna aliyetegema kuwa tunaweza kuwa na Rais mwanamke na akaongoza,” anasema.

“Wanawake wasiogope kufeli kwani unapofeli ndipo unapojifunza zaidi na ikumbukwe kuwa michezo sasa hivi ni ajira sio kama zamani ambapo tulidhani michezo ilikuwa ni kwaajili ya kujifurahisha,” anaongeza.

Anasema kupitia soka amepata fursa nyingi ambazo anaamini asingeweza kuzipata endapo asingekuwa kwenye soka.

Fursa hizo ni pamoja na kukutana na watu mbalimbali wenye sifa tofauti kwenye soka na nje ya soka wakiwamo viongozi wa kitaifa na pia ameweza kutembelea nchi mbalimbali ikiwamo nchi takribani zote za Afrika na baadhi ya nchi katika bara la Ulaya na mabara mengine ambako kwake pamoja na mambo mengine safari hizo kwa namna moja ama nyingine zimemsadia katika kuongeza ujuzi na kupata mtandao wa marafiki.

Kuhusu soka la wanawake nchini, Edna anaamini kuwa linapiga hatua ikilinganishwa na miaka ya nyuma kwani yapo mataifa yanakuja nchini kwa lengo la kujifunza ama kushindana na timu za taifa, jambo ambalo linatoa fursa za maendeleo na uchumi kwa ujumla kwa taifa na wananchi.

Anasema viashiria vya kuwa soka la wanawake nchini linakua ni pamoja na timu za taifa za chini ya miaka 17, 20 na wakubwa kufuzu na kufika hatua mbalimbali za mashindano ya kimataifa ingawa bado jitihada zaidi zinahitajika ili kufika mbali zaidi ikiwamo kuchukua Kombe la Dunia.

Ili kuongeza chachu zaidi katika soka la wanawake anasema kuna haja ya kutengenezwa kwa sheria mbalimbali zitakazohakikisha kunakuwapo na ushiriki mkubwa wa wanawake katika soka.

Anapendekeza mojawapo ya sheria hizo ni pamoja na sheria inayozitaka klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu kwa wanaume kuwa na timu za wanawake kama ilivyo kwa baadhi ya klabu hivi sasa.

“Hii itasaidia kuibuliwa kwa vipaji vingi zaidi ambavyo mwisho wa yote vitatumiwa katika timu za taifa, unajua huku mitaani kuna vipaji vingi sana lakini havionekani kwasababu hakuna fursa,” anaeleza.

Anasema madai ya kuwapo kwa malipo madogo kwa wanawake wachezaji na hata makocha yanaweza kuwa yanachangiwa na sababu nyingi ikiwamo muitikio mdogo wa wanawake kwenye soka.

Ingawa anaamini yapo maboresho katika malipo hayo, lakini ni jukumu la wanawake kujitokeza kwa wingi na kuonyesha utayari wao, hatua ambayo pia itasaidia kuwavutia wafadhili wengi katika soka hilo la wanawake.

Edna anasema kama asingekuwa mchezaji ama kocha, basi angekuwa mchambuzi wa soka na si vinginevyo.

Kuhusu dili lake na Biashara United kocha huyo anasema asingeweza kulizungumzia ingawa anadai ili kuajiriwa kwa nafasi mbalimbali zipo hatua kadhaa za kupitia.

“Ni process ndefu hatuwezi kuzungumzia kwa siku moja, kuna vitu vingi sana wahusika wanaviangalia wakiridhika ndipo sasa mnakubaliana,” anasema.

Anasema tangu akiwa mchezaji hadi sasa hivi amekuwa akikumbana na changanoto mbalimbali lakini ameweza kuzikabili na hivyo kutokuwa kikwazo katika kazi zake.

“Kwanza mimi tangu mwanzo nilisema kuwa mwanasoka hakuwezi kukanibadilisha nikawa na muonekano tofauti kwa maana kuwa nilisema nitabaki kuwa mwanamke tu hata kama nitakuwa na nafasi gani kwenye soka,”anasema

“Sijawahi kuondoka kwenye uhalisia wangu na nitabaki kuwa mwanamke na mama. Nikiwa uwanjani nakuwa na mwonekano wa kimazoezi au kimchezo nikiwa nje ya uwanja nakuwa mama. Mpira hauwezi kuniondoa kwenye jinsia yangu.”

Anasema mwanamke anapokuwa uwajani anacheza ama vyovyote vile kuna watu wanamuangalia yeye kama yeye wengine ni kwa kuvutiwa ama kutokuvutiwa na mwananke huyo, hivyo basi wapo watakaoamua kumzomea ama kumshangilia au kumsifia.

“Hautakiwi kuyatilia maana kwa sababu unaweza kusifiwa sana ama kusemwa sana mwisho wake ukashindwa kuhimili ukajiona mzuri sana ukazidisha sifa ama ukakosa kujiamini kisha ukaharibu kila kitu,” anaeleza.

Anaeleza kuwa malipo yake ya kwanza kwenye soka yalikuwa ni Sh500,000 pesa ambazo alifanyia manununuzi ya vitu vyake vya kawaida.

Lakini pesa kubwa aliyopata kutokana na mchezo wa soka ni Sh6 milioni ambayo alipewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwaajili ya kujikimu aliposafiri na timu ya wanawake kama mwalimu kwenda Ujerumani kwaajili ya mashindano.

“Hiyo pesa nilifanyia kitu kimoja kizuri sana ambacho ni kumbukumbu katika maisha yangu na nisingependa kukitaja kitu hicho ila wewe jua tu ni kitu kizuri,” anasema.

Pia anasema amekutana na matukio mengi ya furaha katika soka ila kubwa zaidi ni la mwaka 2020 ambapo akiwa mwalimu wa timu ya taifa wakati wanacheza fainali Cosafa na kufanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Zambia.

“Mwaka jana pia timu ya U17 mimi nikiwa mwalimu tulifuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia, siku tunashindana pale Zanzibar ilikuwa ni kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa kwakweli nilifurahi sana,” anasema.

Edna anasema anapendelea kula wali samaki au ugali dagaa huku kwenye soka la nje akiwa ni shabiki wa Chelsea na kwa nchini yeye ni shabiki wa timu anayootumikia.

Kwa upande wa burudani, Edna anapenda muziki wa dansi la zamani na bendi anazozipenda ni pamoja na Msondo Ngoma, Sikinde, Twanga Pepeta na FM Academia huku wasanii anaowapenda ni pamoja na Barnaba, Q Chief na Asley

Chanzo: Mwanaspoti