Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ebu sikia haya wanayofanya kina Fei Toto kambini!

Fei Toto 9 Goals Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum "Fei Toto"

Wed, 17 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nje ya kile wanachokionyesha wanasoka wakiwa uwanjani, nyuma ya pazia wana maisha mengine kabisa, yanayoweza kukustaajibisha na kuyaona mapya.

Mwanaspoti limefanya utafiti, kutoka kwa wachezaji mbalimbali, ili kuzijua tabia zao, wakiwa nje ya uwanja, zipo zitakazokufurahisha na kukufundisha na pengine kuacha kuwapachika tabia kwa kuhisia kulingana na mwonekano wao.

Kuna wachezaji wengine ni wakimya, jambo ambalo kwa baadhi ya mashabiki wanawatafsiri kama wana viburi, ila baada ya kuusoma utafiti huu utapunguza kuwahukumu.

KIPRE JR - YEYE NA SIMU

Ni kiungo mshambuliaji wa hatari sana anapochanja mbunga kutafuta kuingia ndani ya boksi. Ukitaka kuthibitisha balaa lake muulize kipa Djigui Diarra wa Yanga ambaye amemfunga mfululizo. Unaambiwa kasi yake uwanjani inachangiwa na jambo moja tu, unataka kufahamu ni lipi?

Ipo hivi; Mwanaspoti limezinasa za ndani kabisa kuwa ukitaka kupata ubora uliotukuka kutoka kwa staa huyo basi mnyang’anye simu yake apate muda wa kupumzika ili mwili wake ukae tayari kwa mazoezi.

“Kipre Jr anapenda sana kuongea na simu na akiachiwa yeye anaweza kuwa wa mwisho kulala kwani sio sana kuzungumza na wenzake, anajitenga na muda wote anaongea na simu, lakini asipopata nafasi hiyo ni mwiba kwa wenzake kwani anakuwa amepumzika muda mrefu hivyo kasi yake uwanjani inakuwa sio ya kawaida kwani mazoezini anawakimbiza wenzake na wapinzani ndio wanakiona cha moto,” meneja wa Azam FC, Rashid Mgunya ambaye muda mwingi anakaa nao anasema huku akikiri kuwa staa huyo ni mpole hazungumzi na mtu, hadi ujengenaye mazoea.

YANICK BANGALA - KIONGOZI

Alijiunga na Azam FC baada ya kuitumikia Yanga akiisaidia kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii huku pia akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Shirikisho la Soka (TFF). Bangala anacheza nafasi mbili uwanjani kama kiungo mkabaji na muda mwingine alikuwa anatumika kama beki wa kati.

Sasa anakipiga Azam FC na huu ni msimu wake wa kwanza. Imethibitishwa kuwa licha ya kazi yake uwanjani kama mchezaji ni kiongozi kwa wachezaji wanzake.

“Ni kiongozi anapenda kuelekeza sana mazoezi, anawaangalia sana wenzake akiona kuna mtu alikuwa bora na kiwango kinashuka ana utaratibu wake wa kumuita na kumkalisha ili ajue shida nini na kumsaidia aweze kurudi mchezoni hivyo kwangu namchukulia kama kiongozi,” anasema Rashid.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO' - MZEE WA 'COVER SONGS'

Ni kinara wa upachikaji wa mabao kwa Azam pia akishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga mwenye mabao 14. Fei Toto ameweka kambani mabao 13. Ufundi wake uwanjani unatokana na kumaliza stresi zake zote nje ya uwanja kwa kuwachekesha wenzake pia anapenda kuimba nyimbo za wasanii mbalimbali.

“Fei Toto ni comedian sana. Anapenda utani, kuimba na utani wake anataka azingatiwe kwani akiona anaowachekesha wanafanya mambo mengine anaharibu kile wanachokizingatia ili asikilizwe yeye kwanza,” anasema na kuongeza;

“Muda mwingine anacheza ‘game’ na kulala hivyo vitu lazima avifanye. Kwa siku mnaweza mkawa mmekaa labda mnaangalia TV anaibuka anaibua mada ya kuchekesha, akiona hamzingatii basi hiyo TV itazimwa,” anasema.

GIBRILL SYLLA - MAZOEZI SANA

Msemo wa usimlazimishe punda kunywa maji una maana pana sana na kwa Gibrill wala haumuhusu kwani mkali huyu kasi yake ya kucheza soka hatumii kazi kubwa kwani anaipenda kazi yake. Nje ya mazoezi ya kocha wao Youssouf Dabo, yeye ana mazoezi binafsi.

“Wakati wengine wako ‘busy’ kupumzika wakicheza game, wengine wakiwa wamelala winga Sylla anakuwa zake kwenye mazoezi binafsi, anapenda sana mazoezi na muda mchache anatumia kulala kupumzisha mwili na wakati mwingine kucheza game,” anasema.

YAHYA ZAYD - SINGELI, MNANDA

Ni kiungo msambuliaji wa zamani wa Ismaily ya Misri na sasa anakibonda pale Azam FC. Staa huyu unaambiwa fanya vyote usifute nyimbo za singeli kwenye simu yake kwani ndio burudani pekee inayompa furaha awapo kambini.

“Ukiachana na matani na uchekeshaji alionao Zayd, anapenda muziki, muda wote akiwa kwenye mapumziko chumbani kwake au eneo lolote atakalochagua kukaa hata akiwa anacheza game basi muziki wa singeli na mnanda lazima usikike,” anasema Mgunya ambaye ni meneja wa timu ya Azam FC.

PASCAL MSINDO - KOMEDI WA TIMU

Ni zao la timu ya vijana. Wanasema jasiri haachi asili hivyo ndio unaweza kusema pamoja na kupata nafasi ya kucheza timu kubwa humwambii kitu kuhusu timu ya vijana kwani muda mwingi anautumia huko kuwapa elimu na njia za kufanya ili waweze kuwa bora.

“Pia ni mchekeshaji anapenda masihara utani ukikutana naye hata kama ulikuwa na hasira mbele yake utapata tabasamu kama sio kicheko kwani utani wake ni wa kufurahisha akipata nafasi anapenda kucheza game.” Anasema.

LUSAJO MWAIKENDA - KOCHA MCHEZAJI

Ubora wake awapo uwanjani umeushawishi uongozi wake kumuongeza mkataba wa miaka miwili itakayomfanya kuendelea kuhudumu kwenye viunga vya timu hiyo hadi 2027. Huyu jamaa nje ya uwanja ni mwalimu mzuri kwa wenzake.

“Nidhamu aliyonayo uwanjani anaiendeleza hadi nje ya uwanja, ni mchezaji ambaye kila mtu ni mkubwa kwake hata akimzidi umri kwani anamuheshimu kila mtu, ni mpole ana heshima anapenda kuwa karibu na timu ya vijana kutoa darasa maana hiyo ndio njia aliyopita na ni kiongozi mzuri, pia akiahidi jambo ni lazima alitimize,” anasema.

ABDUL SULEIMAN ‘SOPU’- SHEIKH WA AZAM FC

Unaambiwa Sopu sehemu ambayo anavaa uso wa kazi ni uwanjani tu akiwa anatekeleza majukumu yake lakini nje na hapo ni mtu wa aibu hawezi kujichanganya na watu, muda mrefu yeye mtu wa ibada (swala)..

“Ndiye mtu ambaye mara nyingi anatumika kwenye kuwaswalisha wachezaji na viongozi wengine wa dini ya Kiislamu kwasababu ni sheikh. Ni mtu wa dini sana na ana aibu sana sehemu hana aibu ni uwanjani tu, kuomba dua kambini ni kitu anakipenda zaidi kuliko kupata muda wa kujichanganya na kucheka na wenzake,” anasema meneja huyo ambaye muda mwingi anakaa na wachezaji.

IDDY SELEMANI ‘NADO’- MZURURAJI

Winga anayewakimbiza mabeki kwa kasi ni mchezaji anayezurura uwanjani hadi kambini kwani yeye hana muda wa kupumzika, anazunguka mabweni ya wachezaji wote kuanzia timu ya wakubwa hadi vijana ukimuhitaji kumpata lazima upate tabu.

“Nado anazurura sana kambini na ni mtu ambaye simu kwake sio kipaumbele kabisa kwani huko anakoenda simu huwa anaacha ndani na kuna muda anasahau hadi alipoiweka hivyo kumpata ni lazima kazi ifanyike, pia ni mchezaji ambaye anajitoa sana ni ana huruma huwezi ukatoka mtupu ukimuambia shida zako ambazo zinahitaji fedha, kama anayo ni anatoa hivyo ni mtoaji.” anasema.

AYUB LYANGA - ANA AIBU SANA

“Kama kuna mchezaji anawapa tabu hadi makocha ni Ayubu, ukimya wake umekuwa ukiwapa shida wakiamini kuwa ni jeuri lakini wakimzoea ni moja ya wachezaji ambao wanakubalika zaidi kwani hana mambo mengi yeye kazi kazi.” anasema na kuongeza;

“Sio makocha tu hadi wachezaji wenzake na hata ninyi waandishi mnahisi kuwa anaringa au jeuri, hapana huyu ni mtaratibu sana na hana mambo mengi yeye ukimuelekeza kitu anafanya kimya kimya muda wake mwingi ni kucheza game akiwa mapumziko,” anasema.

ADOLF BITEGEKO

Ni kiungo aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea timu ya Volsungur IF ya nchini Iceland, sio mtu wa kujichanganya sana na wenzake ni mchezaji ambaye anajielewa sana kwani ameandaa ratiba yake siku hadi siku na ana misimamo yake kama leo alipanga kufanya kitu fulani anahakikisha kimekamilika na akishindwa kukamilisha anakosa amani.

“Pia ni mchezaji ambaye anapenda sana kusoma vitabu, chumba chake huwezi kukosa vitabu, ni mtu wa mazoezi sana mbali na program ya mwalimu pia ana ratiba zake binafsi za mazoezi, na kama ratiba yake ni kwenda kanisani hata kukiwa na programu ya mazoezi hatahudhuria anatoa udhuru aende kwenye ibada na kuandaliwa program yake binafsi,” anasema.

MOHAMED MUSTAFA - SOKA NA KUSWALI

Ni kipa ambaye anacheza kwa mkopo wa miezi sita akitokea El Merreikh, amekuwa bora langoni mwa timu hiyo tangu alipojiunga nayo basi unaambiwa hana habari na mtu.

“Ni mpole sana anapenda utulivu sio mtu wa kujichanganya, akiwa na wakati mzuri anachagua zaidi kuswali na kupumzika kwa kulala,” anasema.

YEISON FUENTES

Lugha pia inaweza kuwa tatizo kwani sio mtu wa stori na mtu yeye muda wote na mambo yake ukimuongelesha anakujibu ukikaa kimya na yeye ananyamaza.

“Anazungumza Kifaransa tu hivyo muda mwingi ananyamaza anakosa mtu wa kuzungumza naye, yeye Kiingereza hakipandi sana.”

Chanzo: Mwanaspoti