Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EURO 2024: Polisi kazi wanayo, mashabiki wanakunjana popote pale

Mashabiki Ugomvi EURO 2024: Polisi kazi wanayo, mashabiki wanakunjana popote pale

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano ya EURO 2024, inazidi kushika kasi. Timu zinapambana kusaka tiketi ya kufuzu mtoano, lakini huko mashabiki wao nao hawajatulia.

Matukio ya vurugu ndani na nje ya uwanja zinazowahusu mashabiki ni nyingi. Polisi wana kazi ya kufanya kutuliza mambo na kila siku mapya yanaibuka, iwe baa, barabarani au uwanjani. Polisi kazi wanayo.

Haya hapa matukio ya vurugu za mashabiki kwa mashabiki na mashabiki na polisi yaliotokea hadi sasa kwenye Euro huko Ujerumani katika miji na mitaa mbalimbali inakofanyika.

BAA

Saa chache kabla ya mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Ujerumani dhidi ya Scottland, inadaiwa mashabiki wa timu hizo walikunjana mashati baa.

Ilikuwa hivi. Jumatano ya wiki iliyopita, saa 3:30 usiku katikati ya Jiji la Munich, maeneo ya Marienplatz, watu wawili (mashabiki wa Ujerumani) waliwashambulia mashabiki wa Scottland.

Taarifa ya Daily Record inaeleza kulikuwa na mzozo baina ya watu hao na kundi la mashabiki wa Scottland kabla ya hali kutulia kwa Wajerumani hao kuondoka, kabla ya kurejea baada ya muda na kuanza tena vurugu kwa kuwarushia viti na kuwapiga na glasi za pombe, huku mashabiki wa Scottland nao wakijibu mapigo.

Hata hivyo, polisi walifika eneo hilo na kutuliza fujo kwa kuwakamata mashabiki hao wawili wa Ujerumani na baadhi wa Scottland.

POLISI APIGWA SHOKA

Polisi mmoja wa doria katika Jiji la Hamburg alinusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa shoka na shabiki mmoja ambaye hajafahamika ni wa nchi gani, saa 6:30 mchana.

Tukio hilo ambalo lilitokea mitaa ya Reeperbahn inaelezwa baada ya kumshabulia polisi huyo, zilifanyika jitihada za kumzuia kabla ya kulazimika kutumia risasi ili kumwokoa polisi huyo.

Baada ya kupigwa risasi, shabiki huyo aliwahishwa hospitali anakoendelea kupatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi la Humberg ilisema; "Kwa mujibu wa taarifa, mwanaume huyo alikuwa akitishia kuwadhuru askari kwa shoka na silaha nyingine, hivyo ili kumtuliza ndio wakatumia bunduki zao, mtu huyo alijeruhiwa na sasa anapatiwa matibabu hospitalini."

Mtaa huo ni moja ya mitaa maarufu katika jiji hilo na mashabiki wa Poland na Uholanzi wako wengi kutokana na jiji hilo kuwa mpakani na nchi hizo na kuingia kwa treni ni dakika chache.

UWANJA WAVAMIWA

Kundi kubwa la mashabiki liliruka mageti na kuvamia uwanja saa chache kabla ya mchezo wa ufunguzi kwenye dimba la Allianz Arena, kati ya Ujerumani dhidi ya Scottland baada ya kuambiwa uwanja umejaa na uuzwaji wa tiketi umesitishwa.

Kundi kubwa la mashabiki lilipanga mstari wa kuingia uwanjani kuanzia saa 5:00 asubuhi, lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya uwanja kujaa na mashabiki waliokosa tiketi waliendelea kuwepo uwanjani hapo hadi saa 3:00 usiku.

Usiku ulipoingia na mchezo kukaribia kuanza, mashabiki hao walipanda fensi na kuvunja mageti ya kuingilia licha ya milango kufungwa.

Inadaiwa kulikuwa na purukushani nyingi kwenye mchezo huo nje ya uwanja na hata vyakula na vinywaji vilivyokuwa vinauzwa uwanjani huduma zilikuwa ndogo na watu walisimama kwenye foleni kwa muda mrefu.

VURUGU UWANJANI

Kabla ya mchezo wa Uturuki dhidi ya Georgia kwenye Uwanja wa Westfalenstadion, ugomvi mkubwa uliibuka baina ya mashabiki wa mataifa hayo.

Picha mbalimbali zilionyesha maji yakimwagika kutoka kwenye paa kushuka sehemu ya jukwaa kulipokuwa na mashabiki na ghafla walianza kupigana na kurushiana vitu, licha ya kutenganishwa na uzio wa chuma.

Baada ya vurugu hizo walinzi walisogelea eneo la tukio na kutuliza ghasia hizo zilizoanza saa moja kabla ya mchezo na kulikuwa na wasiwasi mchezo huo ungechelewa kuanza lakini kila kitu kilienda sawa na ulimalizika kwa Uturuki kushinda mabao 3-1.

Chanzo: Mwanaspoti