Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EPL kuna kitu kinatokea

GHP HAALAND NUNEZ 16 9 EPL kuna kitu kinatokea

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Gumzo ni Bukayo Saka, kwamba amefikia ubora wa kutajwa kama mchezaji wa kiwango cha dunia au bado hajafika?

Maoni ni mengi, lakini Rio Ferdinand, anasema staa huyo ni mzuri, anacheza vizuri, lakini bado hayupo kwenye ubora wa viwango vya dunia.

Rekodi za kwenye Ligi Kuu England zinaonyesha, Saka amecheza mechi 160, amefunga mabao 44, asisti 33 na mashuti 335. Achana na hiyo ishu ya Saka, hebu tuhamie kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England kwa mechi zilizopigwa wikiendi hii.

Kwenye ligi hiyo, kulishuhudiwa mechi za wiki ya 26 – ambapo kulikuwa na matokeo ya kufurahisha na kuumiza kwa baadhi ya timu.

Liverpool yapindua meza kibabe

Liverpool chini ya kocha Jurgen Klopp, imeendelea kuonyesha kwanini ni timu tishio kwenye Ligi Kuu England msimu huu kutokana na kile inachokifanya ndani ya uwanja.

Kwenye mechi yao ya 26 katika Ligi Kuu England, Liverpool ilikipiga na Luton Town na ghafla waliduwazwa baada kutangulia kufungwa. Lakini, Liverpool ilionyesha ubabe wake, ikipindua meza na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Ushindi huo ulidhihirisha ubora wa timu hiyo licha ya kwamba ilicheza bila ya huduma ya wakali wake kadhaa akiwamo Mohamed Salah na Alisson. Liverpool iliweza kutanua pengo la pointi kileleni na kufikia nne, huku ikivuna pointi 22 msimu huu kutoka kwenye mechi ambazo ilianza kufungwa kisha ikashinda kama ambayo imeifanya Luton Town.

Crystal Palace yakimbia kushuka

Katika mechi ya kibabe sana, Crystal Palace ilipata ushindi wa kushawishi wa mabao 3-0 dhidi ya Burnley, wakianza vyema chini ya kocha wao mpya Oliver Glasner.

Mechi hiyo ilifanyika Selhurst Park, si tu ilikuwa mtihani kwa kocha Glasner kujaribu mbinu zake, bali pia ilikuwa muhimu kwa Palace kujiweka mbali na shimo la kushuka daraja.

Burnley ilijiweka kwenye wakati mgumu baada ya kubaki 10 uwanjani kufuatia Josh Brownhill kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Jefferson Lerma.

Matokeo yamewaacha Burnley kwenye hali mbaya, wakishika nafasi ya pili kutoka mkiani. Palace sasa ipo kwenye nafasi ya 13 katika msimamo, pointi nane juu ya timu tano za mkiani.

Aston Villa yasaka tiketi ya Ulaya

Ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Villa Park, Aston Villa iliongeza kasi na kujiimarisha kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England kwa kuibuka na ushindi mtamu kabisa dhidi ya Nottingham Forest wa mabao 4-2.

Kwa ushindi huo, Villa imeweka pengo la pointi tano kwenye nafasi ya nne, dhidi ya Tottenham iliyopo kwenye nafasi ya tano, huku kocha Unai Emery akijaribu kupambana kuhakikisha timu hiyo inanyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kuhakikisha wanaendelea kuwamo kwenye Top Four ili kutimiza hilo.

Ushindi uliifanya Aston Villa kufikisha pointi 52, pointi sita nyuma ya Arsenal waliopo nafasi ya tatu.

Man United shida iko palepale

Katika kipute kilichofanyika Old Trafford, Fulham ilikwenda kupata ushindi maarufu dhidi ya Manchester United kwa bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Alex Iwobi kwenye dakika ya 97, hivyo kushinda kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo tangu mwaka 2003.

Wakati ikiaminika kwamba Man United ingetumia fursa ya Tottenham kutokuwa na mechi wikiendi hii ili kuwafikia kwenye msimamo, lakini kilichotokea ni kile kile cha kupoteza mechi kichapo cha mabao 2-1.

Fulham ilitangulia kufunga kupitia kwa Calvin Bassey kabla ya Harry Maguire kusawazisha na kuonekana kama mechi ingemalizika kwa sare, hadi hapo Adama Traore alipomtengenezea bao Iwobi. Man United sasa imebaki na pointi zao 44 kwenye nafasi ya sita.

Everton inapambana na hali yake

Kwenye timu tatu za mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu England, Everton ipo juu kwa pointi moja tu kwenye hatari ya kuangukia kwenye shimo la kushuka daraja. Wikiendi ilikuwa na mechi ngumu huko Amex, ilikokwenda kukipiga na Brighton na hakika Everton ilipambana na kupata sare ya bao 1-1, ambayo imewafanya kufikisha pointi 21 kwenye nafasi ya 17.

Everton ilikuwa inashinda mechi hiyo hadi hapo Brighton iliposawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Lewis Dunk kwenye dakika tano za mwisho za mchezo.

Brighton, ambayo yenyewe inapambana kupata nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, ilimaliza mechi ikiwa pungufu baada ya Billy Gilmour kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu Amadou Onana. Everton ilitangulia kufunga kupitia kwa Jarrad Branthwaite.

Man City yafukuza mwizi kimyakimya

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City ni kama vile hawapo kwenye ubora mkubwa kwa siku za karibuni, lakini yenyewe inakwenda mdogomdogo kwenye mipango yao ya kulibeba tena taji hilo. Wikiendi iliyopita, chama hilo la Pep Guardiola lilikuwa ugenini kukipiga na Bournemouth na kufanikiwa kushinda 1-0, shukrani kwa bao la Phil Foden.

Man City ilihitaji kushinda mechi hiyo ya ugenini ili kupunguza pengo la pointi ibaki moja baada ya Liverpool kulitaniwa na kuwa nne baada ya ushindi wao kwa Luton Town.

Lakini, kwa sasa, wakati kila timu ikiwa imecheza mechi 26, Liverpool na Man City zimetofautiana pointi moja tu, hivyo kufanya vita ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kuwa ya kibabe zaidi. Nani atashinda vita ni suala la kusubiri na kuona.

Arsenal iko siriazi na biashara yao

Kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, Arsenal ilishindwa hatua za mwishoni kabisa kunyakua taji hilo wakati ilipopigwa kikumbo na Manchester City.

Msimu huu, miamba hiyo inayonolewa na Mhispaniola, Mikel Arteta imeonekana kuwa siriazi kwenye mipango yao ya kunyakua taji hilo baada ya kuhakikisha kwamba hawaachwi mbalimbali na timu inayoongoza na kwa sasa pengo ni pointi mbili tu. Kinachovutia kuhusu Arsenal ni kwamba haishindi kwa kubahatisha, inafunga mabao mengi wapinzani, huku wakiamini kuna wakati Liverpool na Man City zitazubaa na wao watapita kwa kasi kubwa na kukamatia usukani wa msimamo wa ligi hiyo.

Wikiendi ilikipiga na Newcastle United moja ya timu ngumu kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa Arteta na Arsenal yake, wapinzani hao hawakuwa wagumu, wakakubali kichapo cha mabao manne, huku Kai Havertz na Bukayo Saka walikuwa miongoni mwa mastaa walitikisa nyavu katika mechi hiyo.

Wolves kuna kitu wanataka

Wolverhampton Wanderers iliibuka na ushindi finyu wa bao 1-0 dhidi ya Sheffield United, wakitimiza ushindi wao wa 11 msimu huu na hapo kuhakikishia kubaki kwenye Ligi Kuu England.

Kwa bao hilo la Pablo Sarabia katika mechi iliyofanyika uwanjani Molineux, uliisaidia Wolves kushika nafasi ya nane kwenye msimamo, pointi moja tu nyuma ya timu inayoshika nafasi ya saba, Brighton, wakichochea nafasi yao ya kufukuzia tiketi ya kucheza moja ya michuano ya Ulaya kwa msimu ujao.

Kipigo pia kimeiacha Sheffield United kwenye wakati mgumu zaidi, ikiendelea kubaki mkiani kwenye msimamo wa ligi, huku ikishuhudia kupoteza mchezo wao wa 19 msimu huu na kuzidi kuweka hofu ya kushuka daraja na kucheza Championship msimu ujao.

Kama Sheffield United itashindwa kubadilika, basi kuna uwezekano ikarejea ilikotoka kwa kushindwa kupambana kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Chanzo: Mwanaspoti