Mchezaji wa Newcastle United, Alexander Isak ameingia katika orodha ya wachezaji wa Ligi Kuu England ambao nyumba zao ziliwahi kuvamiwa na majambazi kwa miezi ya hivi karibuni.
Nyumba ya Isak ilivamiwa saa 48 tu kabla hajacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Fulham ambapo Newcastle ilishinda bao 1-0 wikiendi iliyopita.
Miezi mitatu iliyopita mchezaji mwenzake Joelinton naye alivamiwa na majambazi ingawa katika matukio yote hayo hakuna mtu aliyetekwa.
Hii pia imewahi kuwatokea wachezaji wengine kama Jack Grealish, Raheem Sterling na Alex Oxlade-Chamberlain.
Majambazi hao mara nyingi huwa wanavamia nyakati ambazo wanafahamu kuwa wachezaji husika watakuwa na timu kwa ajili ya kucheza mechi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Alhamisi ya wiki iliyopita na haijajulikana kama Isak au mmoja kati ya watu wa familia yake walikuwa kwenye mjengo huo uliopo Northumberland wakati tukio linatokea.
Baada ya kuwasili Askari walithibitisha kwamba kuna gari limeibwa katika uvamizi huo lakini bahati nzuri walilikuta limetelekezwa maeneo ya Dissington, maili kadhaa kutoka eneo la tukio.
Mmoja kati ya majirani aliliambia gazeti la The Sun wikiendi iliyopita kwamba: “Maaskari walifika kwenye mjengo huo wakiwa na mbwa ili kufanya uchunguzi wa kina zaidi.”
Hadi sasa haijajulikana ni gari gani liliibwa na kutelekezwa ingawa Isak, ambaye amefunga mabao 19 ya michuano yote tangu kuanza kwa msimu huu, Ijumaa ya wiki iliyopita aliwasili kwenye uwanja wa mazoezi wa Newcastle akiwa na ndinga lake aina ya Mercedes G-Class wagon.