Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EDO: Simba? Siwezi kuisahau kabisa

Edo Pic Data EDO: Simba? Siwezi kuisahau kabisa

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIMBA na Yanga ni timu ambazo kila mchezaji hapa nchini ana ndoto ya kuzichezea. Ni kutokana na umaarufu wa klabu hizo kongwe na idadi ya mashabiki na uhasama kati yao.

Wengi wamepita kwenye klabu hizo na huko wamejifunza mengi na wapo waliofanikiwa kwa kufanya makubwa na kutengeneza maisha yao na familia zao.

Mmoja wa nyota aliyewahi kupita katika moja ya klabu hizi ni aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Edward Christopher ‘Edo’ anayekipiga kwa Wagosi wa Kaya ‘Coastal Union’ kwa sasa baada ya kujiunga nayo akitokea Ruvu Shooting.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano na Edo na kukiri amepita timu nyingi, lakini thamani ya maisha yake ya soka alianza kuyaona akiwa Simba na anajivunia kuwa mmoja wa walioitumikia klabu hiyo inayofanya vizuri kwa sasa kimataifa ikiwa kinara wa Kundi A la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MAISHA NDANI YA SIMBA

Anasema akiwa Simba amepata mafanikio makubwa ikiwamo kuisaidia familia yake na kufungua biashara inayomwingizia kipato nje ya soka na mengi ambayo hajayaweka wazi.

Edo anasema, “Simba ilinifundisha maisha, namna ya kukaa na wenzangu na mambo mengi sana ambayo mpaka hivi sasa najivunia nayo hapa nilipokuwa hivi sasa. Pia imesaidia sana kujulikana na watu.”

Anakiri ukubwa wa klabu hiyo unakufanya ujivunie tofauti na klabu nyingine;

“Hizi timu nyingine kwanza unacheza na mawazo. Wakati mwingine unacheza huku huna pesa na muda wa mshahara umefika hujalipwa ila unakomaa. Lakini Simba hakuna kitu kama hicho tena, unaweza kusahau habari za mshahara kutokana na marupurupu unayoyapata ndani ya timu.”

HATOMSAHAU MILOVAN

Mserbia Milovan Cicovic ni mmoja wa makocha Edo anajivunia kuwa chini yake na amefunguka;

“Siweziu kumsahau. Milovan aliniona nikiwa Simba B, akanipa nafasi ya kucheza timu ya wakubwa. Nafasi hiyo niliipokea kwa mikono miwili na niliifanyia kazi kweli kweli, siwezi kumsahau alinifanya Edo nikajulikana.”

NYOTA WANAOMKOSHA SIMBA

Ligi Kuu Bara ina wachezaji wengi wenye uwezo tofauti tofauti, kwa upande wake Edo anakiri kuwakubali sana Luis Miquissone, Larry Bwalya, Clatous Chama na Prince Dube kutoka Azam.

“Kwa mchezaji anayefuatilia ligi na kujua soka, hawezi kuyaacha majina haya. Aisee hawa watu wanaujua vizuri mpira,” anasema Edo na kufichua, amekuwa akijifunza mengi kutoka kwao na anaamini akipata nafasi ya kukutana nao atapata mengi zaidi.

Anasema wachezaji wa kigeni ni wazuri na wamekuwa wakiwapa changamoto wazawa na mambo mengine adimu.

CHANGAMOTO

“Soka la Tanzania lina changamoto sana na mchezaji asipokuwa na moyo mgumu, anaweza akapoteza ndoto zake.”

Anaanza kwa kusema na kusisitiza kwa upande wake changamoto hizo zimemfunza mengi na kuona ni kama ‘Kumpiga teke chura’ kwani zimemtoa sehemu moja hadi nyingine na nidhamu ndio siri kubwa ya kuwa kwa muda mrefu kwenye soka, akiamini bila ya nidhamu katika kila kazi unayofanya ujipatie kipato ni kazi bure.

AITAMANI STARS

Kati ya mambo anayojivunia Edo ni kuwahi kuitumikia timu ya Taifa, jambo analoamini hakuna mchezaji asiyetamani.

“Nilipata nafasi ya kuitwa Kilimanjaro Stars. Namshukuru sana Mungu kwani ilikuwa ni heshima kubwa sana kwangu. Nawasihi waliopata nafasi kipindi hiki wapambane sana.”

“Kwa sasa kuna wachezaji chipukizi wanakuja kwa kasi na wana uwezo, sijasema wale wa zamani hatuna uwezo, hapana, kinachotizamwa ni ingizo jipya kwa masilahi ya Taifa, ila ikitokea nikapata nafasi uwezo na nia bado ninayo,” anasema.

USHINDANI LIGI KUU

“Namshukuru sana Mungu nimebahatika kucheza ligi misimu mingi, naijua vilivyo, ila misimu hii miwili kumekuwepo na ushindani hasa kwa timu za Simba, Yanga na Azam.”

Anasema amejiunga Coastal Union dirisha dogo na ana imani ataisaidia kufikia malengo ndani ya msimu huu kwa kushirikiana na wenzake kutokana na Kocha wake, Juma Mgunda kumwamini.

KITU ASICHOKISAHAU

Katika maisha yake ndani na nje ya soka, Edo anasema hapendi kusingiziwa au kupakaziwa mambo ambayo hajayafanya ili mradi kumchafua.

“Siwezi kusahau nilisingiziwa mimi eti mlevi mara wanawake, wakati hakuna kitu kama hicho sema watu tu wanakaa na kuamua tumzushie hiki basi niliumizwa sana na wakati huo, ila nikapotezea na maisha yanasonga,” anasema.

NENO KWA BODI

Edo anaishukuru Bodi ya Ligi Kuu Bara kwa kuwathamini wachezaji na kuvifungia viwanja vilivyoonekana kutokuwa na ubora, kwani vimesababisha wachezaji kupata majeraha.

“Wachezaji tunaumia sana tukicheza katika viwanja vibovu basi tu, ni Mungu anatusimamia tunadunda tu, ila kiukweli Bodi na TFF wanatakiwa kuwa wakali ili wamiliki wa viwanja waweze kuvitengeneza na kuwa na ubora,” anasema.

HISTORIA YAKE

Edo alianza kusakata soka akiwa na timu za mtaani, baada ya hapo akajiunga na Moro Kids kabla ya kutua Makongo, Yanga B, Moro United B, Simba, Polisi Morogoro, Toto Africans, Kagera Sugar, Ruvu Shooting na sasa Coastal Union.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz