Staa wa Tottenham Hotspur, Yves Bissouma amepuliziwa gesi ya machozi usoni na wezi na kumpora saa yake yenye thamani ya Pauni 260,000 katika tukio la kushtukiza wakati alipokuwa mapumzikoni na familia yake huko Ufaransa.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Mali alifikia kwenye hoteli ya nyota tano huko Cannes akiwa ameambatana na mkewe, lakini tukio hilo lilitokea nje ya hoteli hiyo ya Majestic Barriere, Jumapili asubuhi.
Bissouma alikutaka na vibaka hao wawili waliokuwa wamevaa maski, wakati anateremka kwenye gari yake Promenade de la Croisette.
Wakati akielekea kwenye mlango wa hoteli, ndipo kibaka mmoja alipomsogelea na kumpulizia gesi ya machozi usini na kumwibia saa yake ya Pauni 260,000 na kisha kutokea kusikojulikana wakiwa na gari tofauti.
Polisi wa Ufaransa wafanya uchunguzi juu ya jambo hilo, huku Bissouma na mkewe wakirejea London, England na kukatiza mapumziko yao.
Staa huyo hakupata majeraha yoyote kwenye tukio hilo, isipokuwa alipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na shambulizi la kushtukiza.
Msemaji wa Spurs alisema: “Tunafahamu tukio lililomtokea Yves, hivyo tunaendelea kumfuatilia hali yake na familia.”
Bissouma alijiunga na Spurs wakati wa dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 30 milioni akitokea Brighton, ambako alicheza kwa misimu minne.
Wachezaji wengine wa Ligi Kuu England waliolizwa na vibaka ndani ya miezi 12 iliyopita ni pamoja na Jack Grealish, Alexander Isak na Kurt Zouma.