Bingwa mtetezi wa Michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), Yanga itashuka uwanjani leo kukabiliana na Tanzania Prisons katika hatua ya 16 ya michuano hiyo.
Yanga inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na alama 62, imefunga jumla ya mabao 42 huku mabao 15 yakifungwa na Fiston Mayele ambaye ndiye kinara katika safu ya ufungaji wa ligi.
Tanzania Prisons inashika nafasi ya 14 imefunga mabao 18 huku wachezaji wake wote wakifunga mabao 16 na mabao mawili wakiyapata kutokana na mpinzani kujifunga, Shawn Oduro (Geita) na Frank Magingi (Namungo).
Mchezaji mwenye mabao mengi upande wa Tanzania Prisons ni Jeremiah Juma mwenye mabao matano, Samson Mbagula mabao manne, Ismail Ismail Juma, Ismail Mgunda, Oscar Paul, Khamis Mcha, Jumanne Elfadhil, Zabron Khamis na Zabona kila mmoja anabao moja.
Hivyo kikosi kizima cha Tanzania Prisons kimekusanya mabao 18 ambayo ni sawa na mabao 18 yalifungwa na washambuliaji wawili wa Yanga, Mayele (15) na Clement Mzize mabao matatu.
Yanga inakutana na Tanzania Prisons ambayo haina rekodi ya ushindi dhidi yake kwani katika michezo 20 zilizokutana Wajelajela hao wameambulia alama tatu mara moja pekee. Katika michezo hiyo Yanga imepoteza mchezo mmoja uliopigwa
Sokoine, Mei 10, 2018 ikifungwa 2-1, suluhu michezo miwili huku ikishinda michezo 12 na sare ya mabao michezo mitano. Kocha wa Prisons, Abdalah Mohamed 'Bares' anakiri kuwa kwenye hali tete ndani ya kikosi chake kutokana na matokeo mabovu wanayokutana nayo kwenye ligi.
"Nimekuwa nikikizidi kufanya mbadiliko ya kila wakati ili kuona namna ya kupata matokeo mazuri lakini bado tunakabiliwa na changamoto za hapa na pale.
"Tunakutana na Yanga sio mchezo rahisi kwetu kutokana na uimara wa mpinzani wetu lakini tunakwenda kukabiliana nao hadi dakika ya mwisho," alisema Bares. Mchezo wa mwisho kukutana timu hizo Dar es Salaam ilikuwa Mei 9 mwaka jana, Uwanja wa Mkapa na kutoka suluhu lakini mchezo wa kwanza msimu huu Uwanja wa Sokoine, Prisons ilichapwa mabao 2-1.
Baada ya kumalizana kwenye ASFC timu hizo zitakutana tena kwenye mchezo Ligi Kuu wa kufunga msimu Mei 28 mwaka huu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ikumbukwe tangu kuanzishwa kwa mashindano haya mwaka 1967 Yanga, ndio timu iliyobeba makombe mengi (6) na tangu yaliporejeshwa mwaka 2015 imebeba mara mbili, msimu wa mwaka 2015/16, ikiichapa Azam 3-1 na msimu uliopita ikiichapa Coastal Union kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.