Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Duh! Chelsea sasa yapanga kumuuza Mudryk kisa Olise

Oliseeeee Michael Olise

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Chelsea wanafikiria kumuuza winga wao raia wa Ukraine, Mykhailo Mudryk, 23, katika dirisha hili ili wapate pesa watakazotumia kumsajili winga wa Crystal Palace na Ufaransa, Michael Olise, 22, katika dirisha hili.

Olise amekuwa akiwindwa na vigogo wengi barani Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita.

Hata hivyo, kuipata saini yake inaweza kuwa na changamoto kwa sababu timu nyingi kubwa barani Ulaya zinamhitaji na kwa mujibu wa taarifa anaweza kugharimu zaidi ya Pauni 60 milioni.

Mpango wa kumuuza Mykhailo umepitishwa moja kwa moja na viongozi wa Chelsea kwa sababu staa huyu hakuonyesha kiwango bora kwa msimu uliopita licha ya kusajiliwa kwa matarajio makubwa. Mudryk alikuwa anawaniwa na Arsenal lakini akaitosa katika dakika za mwisho.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali timu zinazomhitaji zitatakiwa kutoa zaidi ya Pauni 50 milioni na ikishindikana atatolewa kwa mkopo lakini kwa sharti la timu inayomhitaji kulipa mshahara wake wote.

CHELSEA inataka kumsajili straika wa RB Leipzig na Ubelgiji, Lois Openda, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na inatarajia kukamilisha dili lake baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro au timu yake itakapotolewa.

Openda mwenye umri wa miaka 24, katika msimu uliopita alicheza mechi 46 za michuano yote na katika Bundesliga alifunga mabao 24. Mkataba wake wa sasa unamalizika 2028.

SOUTHAMPTON ipo tayari kulipa hadi Pauni 6 milioni kwenda West Ham kwa ajili ya kuipata saini ya straika wa wagonga nyundo hao, Danny Ings katika dirisha hili.

S’oton ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu England msimu ujao, ina matumaini makubwa ya kumpata Ings ambaye aliwahi kucheza katika kikosi chao, baada ya staa huyo kuonyesha nia ya kuondoka Hammers.

MANCHESTER United inataka kuwasilisha ofa kwenda Genoa kwa ajili ya kumsajili kipa wa timu hiyo na Hispania Josep Martinez, licha ya kipa huyo kuwa tayari ameshafanya makubaliano binafsi na Inter Milan ambayo pia inataka kumsajili.

Kipa huyu mwenye umri wa miaka 26, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2025. Msimu uliomalizika alicheza mechi 36.

EVERTON inahitaji walau Pauni 50 milioni kutoka kwa timu yoyote inayohitaji saini ya kiungo wao raia wa Ubelgiji, Amadou Onana katika dirisha hili.

Onana mwenye umri wa miaka 22, huduma yake imekuwa ikimezewa mate na Arsenal ambayo ipo tayari kutoa kiasi hicho cha pesa ili kukamilisha dili lake.

AJAX imevutiwa na mshambuliaji wa Burnley, Wout Weghorst, 31, ambaye inataka kumsajili katika dirisha hili ikiwa ni sehemu ya kujenga upya kikosi chao baada ya kufanya vibaya msimu uliomalizika. Staa huyu wa kimataifa wa Uholanzi ambaye ameshawahi kuichezea ManUnited, mkataba wake na Burnley unamalizika mwaka 2025. Msimu uliomalizika akiwa na Hoffenheim kwa mkopo, alifunga mabao manane, katika mechi 31 za michuano yote. Dili hilo linaweza kukamilika baada ya fundi huyu kutoka katika michuano ya Euro.

WEST Ham ipo katika hatua nzuri ya kumsajili mshambuliaji wa Sunderland, Jack Clarke, 23, katika dirisha hili baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha staa huyu raia wa England msimu uliopita ambapo alicheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 15. Mkataba wa sasa wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.

IPSWICH, Southampton, Leicester na Leeds zote zimeripotiwa kuanza mazungumzo na Tottenham ili kuipata saini ya beki wa timu hiyo na Wales, Joe Radon, 26, katika dirisha hili.

Radon hajapata nafasi kubwa ya kucheza kwa msimu uliopita na hiyo ndio imesababisha awasilishe barua ya kuomba kuondoka kwa mkopo au auzwe kwenda timu itakayompa nafasi kubwa.

Chanzo: Mwanaspoti