Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dube kuondoka Azam ni baraka iliyojificha

Prince Dube 1 Dube kuondoka Azam ni baraka iliyojificha

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa Kiingereza wanaita blessing in disguise. Kwa Kiswahili ni baraka iliyojificha. Hili ni jambo au tukio chanya linalomfika mtu kama zao la tukio hasi lililotangulia kumkuta.

Kwa mfano, Barcelona walitaka kumsajili David Beckham kutoka Manchester United mwaka 2003, lakini wakazidiwa maarifa na Real Madrid, wakamkosa.

Hili lilikuwa tukio hasi lililowakuta kwa sababu walishazungumza naye kabisa na hadi jezi zake walishachapisha wakisubiri kuziingiza sokoni baada ya kumtangaza.

Baada ya kumkosa wakaenda kumsajili Ronaldinho kutoka PSG. Mungu si Athuman usajili huo ukawapa kitu kikubwa ambacho wasingekipata kwa David Beckham.

Lakini hata hivyo, Ronaldinho alikuwa aende Manchester United, siyo Barcelona. Walishaongea naye na akafunga safari kutoka mjini Paris, Ufaransa hadi mjini Manchester, England.

Bahati mbaya ni kwamba hakupenda hali ya hewa ya mji huo kwani alikwenda wakati wa mvua kali. Akaghairi ndipo akaenda Barcelona. Baada ya kumkosa Ronaldinho, Manchester United wakamsajili Cristiano Ronaldo. Akaenda kuwa msaada mkubwa sana kwao.

Hii yote ni mifano ya baraka iliyojificha au blessing in disguise kama ambavyo wanaita Waingereza. Sasa hali kama hii ndiyo itaenda kuwatokea Azam FC baada ya kuondokewa na Prince Dube, katika njia mbili tofauti.

1. SIYO MFUNGAJI HODARI

Kwa muda mrefu Prince Dube ameimbwa kama mmoja wa washambuliaji hodari kwenye ligi yetu, hii haina shaka. Lakini bahati mbaya namba zake ni za chini tofauti na jina lake.

Dube amecheza Tanzania kwa misimu mitatu na nusu tangu ajiunge na Azam FC, Agosti 2020. Kwa misimu yote hiyo amefunga mabao 34 tu katika mechi 75.

2020/21

-Mabao 14 (mechi 23)

2021/22

-Bao 1 (mechi 14)

2022/23

-Mabao 12 (mechi 26)

2023/24

-Mabao 7 (mechi 12)

Huyu siyo aina ya mshambuliaji ambaye alitakiwa aibebe Azam FC na kuirudisha kwenye njia ya ubingwa. Ukiangalia takwimu za washambuliaji wa wapinzani wao ambao wametwaa ubingwa katika misimu ya hivi karibuni tangu ajiunge na Azam FC, utaona za Dube hazitoshi kuiongoza Azam FC katika mbio za ubingwa.

2020/21:

John Bocco (Simba) - Mabao 16

Chris Mugalu (Simba) - Mabao 15

Prince Dube (Azam FC) - Mabao 14

2021/22

George Mpole (Geita Gold) - Mabao 17

Fiston Mayele (Yanga) - Mabao 16

Reliants Lusajo (Namungo) - Mabao 10

Prince Dube (Azam FC) - Bao 1

2022/23

Fiston Mayele (Yanga) - Mabao 17

Saido Ntibanzonkiza (Simba/Geita) - Mabao 17

Prince Dube (Azam FC) - Mabao 12

Zaidi tu ya idadi ya mabao, Dube pia ana tatizo la kukosa muendelezo wa ufungaji.

Kwa mfano, msimu uliopita (2022/23) alifunga mabao 12, lakini mabao haya yalipıshana kwa umbali mkubwa sana. Alifunga katika siku ya kwanza ya ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Baada ya hapo, hakufunga tena hadi katika mechi ya nane dhidi ya Simba. Na akafunga tena mechi iliyofuata dhidi ya Ihefu ambayo ilikuwa ya tisa ya msimu.

Baada ya hapo hakufunga tena hadi mechi ya 17 dhidi ya Geita kule Nyankumbu.

Kwa hiyo hadi mchezo wa 17 wa ligi alikuwa na mabao manne tu.

Akafunga tena katika mchezo wa 19 dhidi ya Mbeya City. Hii ina maana hadi mchezo wa 19 wa ligi, Dube alikuwa na mabao matano. Huyo hawezi kuwa mshambuliaji wa kuiongoza timu katika mbio za ubingwa. Bao la sita akalifunga kwenye mchezo wa 23, dhidi ya Simba.

Bingwa wa msimu, Yanga, alipatikana Mei 13 baada ya ushindi wa 4-2 dhidi ya Dodoma Jiji. Hadi hapo Dube alikuwa na mabao saba. Akaja kufunga matano kwenye mechi mbili za mwisho za msimu ambazo tayari bingwa alishapatikana na kufikisha 12.

Hoja hapa ni kwamba Dube hakuwa mshambuliaji sahihi wa kuibeba Azam FC katika mbio za ubingwa kwa sababu hakuwa akiamua mechi kibingwa. Mshambuliaji wa ubingwa hatakiwi kucheza mechi hadi saba bila kufunga. Dube alikuwa akifanya hivyo.

Ushahidi ni msimu mmoja kabla ya huo, yaani 2021/22 ambapo alifunga bao moja pekee katika mechi 14. Yaani mshambuliaji afunge bao moja pekee katika mechi 14 ndiyo umtegemee kwenye ubingwa?

2. HUWEZI KUMTEGEMEA

Katika misimu yake mitatu na nusu aliyocheza Tanzania, Dube amekosa mechi 32 za ligi kutokana majeraha. Msimu mmoja wa ligi ya Tanzania una mechi 30, maana yake alikosa msimu mzima kimahesabu kutoka na majeraha.

Kwa hiyo itoshe tu kusema kwamba Dube alicheza uwanjani kwa misimu miwili na nusu huku msimu mmoja akiuchezea kwenye wodi ya wagonjwa.

2020/21

Huu ndiyo msimu wake wa kwanza na ndiyo uliomtambulisha Tanzania kama mshambuliaji hatari. Katika mechi 11 za kwanza alifunga mabao matano huku Azam FC ikianza ligi kwa kishindo na kushinda mechi saba mfululizo.

Mchezo wa 12 wa ligi ulikuwa dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 ambapo aliumia na kuvunjika mkono. Akakaa nje Desemba yote akikosa mechi tano, akapona Januari.

Akacheza mechi 14 salama hadi Juni 2021 dhidi Namungo aliposhindwa kuendelea na mchezo akilalamikia maumivu chini ya kitovu. Alikaa nje hadi Januari 2022 alipoibukia Afcon na timu yake ya taifa ya Zimbabwe.

Katika kipindi hicho alikosa mechi 20 - 16 za ligi na nne za Kombe la Shirikisho la CAF. Hata aliporudi hakuwa tena Dube yule ambaye Watanzania walimuona kwenye mechi saba za kwanza za msimu wa 2020/21.

Msimu huu, 2021/22 Dube alikosa mechi 16 za ligi, akicheza mechi 14 tu na kufunga bao moja. Msimu huo hadi anaandika barua ya kuomba kuvunja mkataba na klabu yake, Dube alishakosa mechi saba kutokana na majeraha. Hadi hapo ligi ilikuwa katika mzunguko wa 19.

Kwa jumla, Dube ameumia mara 36 katika maisha yake ya soka akiwa na Azam FC. Hizi ni rekodi za majeraha makubwa yaliyomfanya akose mechi na madogo madogo ya kukosa mechi chini ya tatu.

Maana yake Dube ameumia mara nyingi zaidi ya mabao aliyofunga ambayo ni 34.

HITIMISHO

Kwa miaka yote hiyo Azam FC walikuwa kwenye usingizi mzito wakiamini wana mchezaji anayeweza kuwapeleka sehemu fulani, lakini ukweli ni kwamba Dube hakuwa aina hiyo ya mchezaji waliyedhani.

Kwa hiyo kuondoka kwake ni baraka iliyojificha ambayo sasa inajitokeza kupitia namba. Na endapo watapata mshambuliaji mwingine ambaye atawapa uhakika wa kuwepo uwanjani mfululizo kama alivyokuwa Mayele wa Yanga ambaye alicheza misimu miwili mfululizo pasi na kupata majeraha, basi itakuwa baraka nyingine.

Azam FC badala ya kuumia kuondokewa na Dube, waone hii ni baraka kwao na wakipata hizo Dola 300,000 ni baraka nyingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: