Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dube katikati ya Fei Toto na Gallas

Prince Dube Ms Dube katikati ya Fei Toto na Gallas

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Imepita zaidi ya miezi mitano tangu kumalizika kwa sakata la mchezaji Feisal Salum "Fei toto' ambaye kwa sasa anaichezea Azam.

Wakati nchi ikiwa inamalizia maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi limeibuka sakata lingine la Prince Dube. Watu wengi wamezoea kumuita mwana mfalme kutoka Zimbabwe.

Huenda ulimwengu wa wapenda soka nchini haujamfaidi vizuri kutokana na 'mahaba yake na kitanda cha wagonjwa'. Inawezekana hakuimbwa sana kwa sababu hachezi timu yenye mashabiki wengi nchini.

Lakini ukienda pale Harare, Zimbabwe, Dube ni mmoja wa wachezaji waliokuzwa kwenye mifupa ya soka ya taifa hilo na wanafahamika vilivyo.

Ndio! Tanzania waliwahi kupita Wazimbabwe kadhaa akiwemo Donald Ngoma ambaye aliwahi kuonyesha kiwango bora akiwa na Yanga, lakini wakati anafanya hayo kuanzia 2015, hakuwahi kabisa kuitwa timu ya taifa ya Zimbabwe.

Mara yake ya mwisho ilikuwa ni kwenye michuano ya Chan. Hakuwahi kunusa harufu ya Afcon ama michuano mingine mikubwa zaidi ya hiyo, licha ya kwamba alionekana kuwa lulu pale Jangwani.

Dube amefanikiwa kuitwa na kucheza Afcon na amekuwa akiitwa kwenye kikosi cha Zimbabwe pale anapokuwa hana majeraha. Kwanini? Ni kwa sababu ni sehemu ya mpango maalumu wa nchi. Aliwahi kukuzwa kuanzia mdogo na kucheza timu mbalimbali za vijana za taifa hilo.

Hivyo, alipofikia umri wa utu uzima ilikuwa ni rahisi kupenya kwenye timu ya wakubwa na kucheza kwa bahati ambayo wachezaji wengi wa ndani hawajaipata, kwa sababu taifa hilo lina utitiri wa mastaa wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Afrika ikiwemo Asia na Ulaya.

Bahati mbaya kwa Azam, Dube ameomba kuondoka taarifa zinakwenda mbali na kueleza amesharudisha karibu kila kitu alichopewa na timu hiyo ikiwemo nyumba ili tu aruhusiwe kuondoka.

Hata hivyo Azam wamemwambia wanataka Dola 300,000 (zaidi ya Sh700 milioni) ili kumuacha aende zake. Mwanaspoti imeripoti kwamba Dube amewasilisha nusu ya pesa hiyo, lakini Azam FC imekataa na kusisitiza kwamba inazitaka zote.

Dube ameonyesha wazi kuwa hataki kuendelea kuichezea timu hiyo na kwamba moyo wake upo sehemu nyingine. Kuna taarifa zinaeleza kwamba Yanga ndio timu anayoweza kujiunga nayo ikiwa ataondoka, ingawa Ihefu pia inatajwa.

Ndani ya siku mbili inaonekana Dube anafanya juhudi zote na kila linalowezekana ili kufanikisha azma yake. Ishu ya Dube inakumbushia tukio la mchezaji wa zamani wa Chelsea na Arsenal, William Gallas.

Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali barani Ulaya ni kwamba, supastaa huyo aliyekuwa moto enzi zake alilazimisha kuondoka Chelsea katika dirisha la majira ya kiangazi 2006, lakini iligoma kumuachia wala kumuuza.

Gallas anaeleza kwamba hakujisikia kuendelea kuichezea Chelsea na alichotaka ilikuwa kuondoka zake Stanford Bridge. Bado mabosi wa Chelsea hawakutaka kumuachia. Alipoona hawamsikilizi akawaambia kwamba atabaki, lakini kama watamchezesha angeweza kujifunga mwenyewe.

Kufikia hapo Chelsea ikaona jamaa ni kweli anamaanisha anachosema, akapelekwa Arsenal katika dili ambalo lilikuwa la mabadilishano ya wachezaji ambapo Ashley Cole alitua Chelsea.

Ukisikiliza ishu ya hawa wawili unakumbuka sakata la Fei Toto unaona ni stori zinazofanana. Wachezaji wote hao waligoma na hawakuwa wanataka kuendelea kuzichezea timu zao.

Ingawa Fei Toto alikuwa akitaka kuona rais wa Yanga, Hersi Said anaondoka ndipo arudi kikosini jambo ambalo lilikuwa gumu na mwishoni aliruhusiwa kuondoka kwenda Azam, kupitia ombi la maalumu lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokutana na Yanga, Ikulu, Dar es Salaam.

Mara nyingi ikishazuka hali kama hii huwa vigumu mchezaji kuendelea kusalia kwenye timu. Wanasema moja ya mambo ambayo mchezaji hutaka kuwa nayo kabla ya kucheza au kuitumikia timu yoyote ni utayari wa kimwili na kiakili. La sivyo ni vigumu kukipiga kwa asilimia mia moja. Filamu ya Dube imeanza tunasubiri kuona mwisho wake.

Chanzo: Mwanaspoti