Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dube ang’oa kifaa Azam FC

Dube Kifaa Dube ang’oa kifaa Azam FC

Tue, 26 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kama ulijua sekeseke la Prince Dube kuondoka Azam litaacha wengine salama, jibu ni hapana kwani klabu hiyo imeachana rasmi na kipa wake raia wa Ghana, Abdullahi Idrissu.

Kipa huyo yupo kwao akijiuguza baada ya kuumia na kufanyiwa upasuaji. Idrissu aliumia Oktoba 27, 2023 dimbani Azam Complex kwenye mchezo wa kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa wauaji wa Kusini, Namungo.

Mwanaspoti linajua alikwenda Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji uliomtaka kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita akijiuguza. Aliporudi nchini akaenda kwao Ghana kuendelea na mapumziko ya kujiuguza, lakini akiwa huko amekutana na THANK YOU yake juu kwa juu za ndaani kabisa zikaeleza kisa ni sakata la Dube.

KWANINI?

Mwanaspoti linajua Abdullahi Idrissu alijiunga na Azam, Januari 2023 akitokea Bechem United ya Ghana. Wakala wa mchezaji huyo pia ni wakala wa Prince Dube, mshambuliaji aliyewatosa Azam wakati msimu huu ukiendelea.

Taarifa za chini kwa chini zinamhusisha Dube kuelekea Yanga, klabu ambayo wakala wa Idrissu na Dube pia anafanya nayo kazi.

Wakala huyo ndiye aliyewapeleka Yanga, Kennedy Musonda kutoka Zambia na Hafiz Konkon kutoka Ghana. Prince Dube, kipenzi cha matajiri wa Azam, aliwashtukiza waajiri wake kwa barua ya kutaka kuvunja mkataba wakati wa vuguvugu la kuelekea mechi dhidi ya Yanga.

Halafu zinakuja taarifa za chini kwa chini kwamba Yanga ndiyo wako nyuma ya sakata la mchezaji huyo kuleta kiburi. Akaunganishwa wakala wake na mahusiano yake na Yanga, kisha ikavutwa picha hadi kwenye mchezo wa Oktoba 23, 2023 kati ya timu hizi mbili.

Katika mchezo huo, Yanga ilishinda 3-2 ikifaidika na makosa ya kipa Abdullahi Idrissu. Kwa hiyo menejimenti ya Azam imehisi kwamba yale hayakuwa makosa ya kibinadamu kwa Idrissu bali kulikuwa na namna.

Na wanamhusisha wakala wa Idrissu na ufanisi mdogo wa kipa huyo kwenye mechi za hivikaribuni huku ikihusishwa pia na ukaribu wake na Yanga.

Na pia habari zinazoendelea kwamba anampeleka Prince Dube Yanga. Huu mzunguko umewalazimisha Azam kufanya hitimisho kwamba wakala yule na vijana wake yaani Dube na Idrissu, hawataendelea kuwepo Chamazi.

Kwa hiyo wameamua kukata mizizi yote. Dube amekaa Azam miaka mitatu na nusu. Katika kipindi hicho, Azam imeifunga Yanga mara moja tu.

Lakini ukirudi nyuma miaka miwili tu kabla ya ujio wa Dube, Azam iliifunga Yanga mara tatu, huku ikipoteza mara moja tu. Tafsiri ya viongozi ni kwamba Azam haikuwa salama mbele ya Yanga katika kipindi cha Dube klabuni hapo.

Na baada ya kuondoka tu, Azam wameshinda dhidi ya Yanga. Hali hiyo imewafanya waamini kabisa kwamba hawakuwa watu sahihi ndani ya timu yao,ndio maana wameamua kuachana na Idrissu.

Dube amekimbia mwenyewe na aliyebaki alikuwa Idrissu ambaye sasa anakutana na THANK YOU yake huko huko kwao bila kujali gharama ambazo klabu itaingia.

DUBE NA YANGA

Inasemekana kwamba ramani nzima ya Dube kwenda Yanga ilichorwa na aliyekuwa mtumishi wa Azam ambaye sasa ni mfanyakazi wa Yanga.

Habari zinasema bwana huyo ambaye majukumu yake ndani ya Azam yalikuwa kushughulika na wafanyakazi wote, ndiye aliyekuwa akikaa na mafaili yote ya wachezaji wa klabu hiyo na amechora ramani yote ya vita.

Na yeye ndiye alikuwa mtu wa karibu zaidi na Dube ukiacha matajiri wenyewe. Habari zinasema yeye ndiye aliyeandika ile THANK YOU aliyoichapisha Dube kwenye mtandao wake wa Instagram kuwaaga Azam.

Mwanaspoti limeambiwa kuwa ukaribu huo ndio uliotumika kurahisisha mawasiliano baina ya Dube na Yanga yakimhusisha wakala wake.

Azam imeyagundua hayo na ikachukua hatua za ndani kuhakikisha wanang’oa mizizi yote.

SAKATA LA DUBE

Mwanaspoti linajua hadi sasa hakuna mpya katika sakata la Dube na Azam kutoka pande zote mbili.

Tangu Dube apeleke barua ya kuomba kuvunja mkataba, hajarudi tena klabuni hapo, zaidi ya kuonekana Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa Azam na Yanga.

Azam nao tangu watoe taarifa ya kupokea ofa kutoka Al Hilal ya Sudan na Simba ya Tanzania, hawajasema kingine chochote .

Taarifa za ndani zinadai ofa hizo mbili zimekataliwa kwa sababu hazijafika kiwango ambacho wao wanakihitaji huku ikielezwa kwamba Simba ilikuwa tayari kutoa dola 300,000 lakini kwa awamu.

Kwa sasa Azam bado haijachukua hatua zozote za kisheria dhidi ya Dube zaidi ya kutompa mshahara wake.

BARUA NANE

Na Azam inafanya hivyo kama mkataba wao na mchezaji huyo unavyosema kwamba anatakiwa kuwepo kazini siku zote ili alipwe mshahara, la sivyo iwepo taarifa rasmi iliyoidhinishwa na uongozi.

Na katika kujiweka salama na hilo, Azam humuandikia barua Dube kila baada ya siku tatu tangu Machi 5 kumtaka aende mazoezini ili ahesabike yuko kazini hivyo alipwe mshahara wake.

Nakala za barua hizo hupelekwa TFF na Fifa kama ushahidi. Azam FC inachukua kila tahadhari ili kesi isije kuwageukia. Japo Dube aliomba kuvunja mkataba, lakini bado anahesabika kama mchezaji wa Azam FC hadi mchakato wa kuvunja mkataba utakapokamilika.

Habari zinasema kutokana na hilo, bado anastahili kupata stahiki zake zote za kimkataba. Lakini ili hayo yawezekane, ni lazima yeye mwenyewe awe kazini na kwa kuwa haendi, basi anakuwa amekiuka yeye na klabu inabaki salama.

Hata hivyo, Mwanaspoti linajua ni lazima klabu ithibitishe kwamba Dube hakuwa kazini na uthibitisho ndiyo hizo barua ambazo anaandikiwa kila baada ya siku tatu.

Mwanaspoti linajua kwamba Dube ameshafikia pazuri na Yanga na wamemuwekea mpaka ulinzi saa 24 Jijini Dar es Salaam na kumpangishia nyumba Masaki ambayo thamani za ndani peke yake ni Sh30Milioni na amekwenda kuchangua mwenyewe dukani.

Mbali na hilo Mwanaspoti linajua watu wa karibu na Yanga wamemuahidi mchezaji huyo mkataba wa miaka miwili na wakamsisitiza atulie wenyewe wanajua jinsi ya kumaliza sakata hilo. Tupe maoni kuhusiana na sakata hili kwa namba yetu.

Chanzo: Mwanaspoti