Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube amesema baada ya kujitafuta kwa misimu miwili bila kufikia rekodi yake, msimu huu anataka kuvunja rekodi ya Fiston Mayele katika Ligi Kuu Bara.
Mayele, mshambuliaji wa zamani wa Young Africans na Saido Ntibazonkiza wa Simba SC msimu uliopita walifunga mabao 17, Dube ana ndoto ya kufunga angalau mabao 18 msimu huu.
Dube msimu huu ni wanne tangu alipojiunga na Azam FC 2020/21 na alitupia mabao 14, 2021/22 alifunga matatu huku 2022/23 akitupia 11 na huu hadi sasa amefunga saba.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Dube amesema sababu ya kutokuwa na mwendelezo mzuri wa upachikaji wa mabao ni kutokana na majeraha ambayo yamekuwa yakimwandama mara kwa mara, ingawa hayamzuii kuinyanyasa Simba SC popote anapokutana nayo uwanjani.
“Nimekuwa nikianza vizuri msimu, lakini ikifika katikati ya msimu nakumbwa na majeraha. Hii hali ndio inanifanya nishindwe kufikia malengo ambayo nakuwa nimejipangia,” amesema Mshambuliaji huyo kutoka nchini Zimbabwe.
“Kazi yangu ni kufunga na hicho ndicho kinanifanıya nikae ndani ya kikosi cha Azam FC. Nimekuwa sifurahishwi na idadi ndogo ya mabao ninayofunga, nimeshindwa hadi kufikia rekodi yangu ya msinmu wangu kwa kwanza, sio nzuri kwangu.”
Akizungumzia kutwaa kiatu cha mfungaji bora msimu huu, amesema nafasi bado ipo wazi, lakini hazingatii zaidi bali anatamani kuvunja rekodi yake mwenyewe kwa kufunga mabao zaidi.
Amesema kwanza anatamani kuvunja rekodi ya msimu wake wa kwanza alipofunga mabao 14 kwa kufunga mabao 18 msimu huu.