Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dube aanza mdogomdogo

Dube Azam.jpeg Mshambuliajji wa Azam FC, Prince Dube

Wed, 6 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji Mzimbabwe wa Azam FC, Prince Dube aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu chini ya tumbo, ameanza kufanya mazoezi mepesi ikiwa ni hatua ya pili kabla ya kujumuika na wenzake kwa ajili ya Ligi Kuu Bara.

Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema Dube amemaliza hatua ya kwanza aliyotakiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu na baada ya hapo ameingia hatua ya pili ya kufanya mazoezi mepesi.

Zaka amesema Dube atakuwa akifanya mazoezi mepesi kwa kufuata programu maalumu kabla ya kuungana wenzake, Oktoba 22.

“Maendeleo ya Dube ni mazuri, hivi karibuni tutamuona akirejea tena uwanjani kuipigania klabu yetu. Kijumla tulisema atakaa nje ya uwanja kwa wiki sita, sasa tayari amemaliza wiki tatu za mwanzo ameingia nyingine ambazo zitakuwa za mazoezi mepesi na baada ya hapo nd’o ataungana na wenzake huku akitazamwa kwa ukaribu,” amesema.

Dube aliyemaliza msimu uliopita na mabao 14 licha ya kucheza kwa muda mfupi kutokana na kuwa majeruhi kila mara, alisumbuliwa na maumivu tangu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora na baada ya kuumia alipelekwa Afrika Kusini kwa Dk Nicolas anayewatibia wachezaji wa Azam FC.

Baada ya vipimo daktari huyo alishauri achomwe sindano bila upasuaji.

Lakini, aliendelea kusumbuliwa na maumivu kabla ya kuanguka na kushindwa kuendelea na mchezo wa kirafiki dhidi ya Kabwe Warriors ambao alifunga na ndipo aliporudishwa Afrika Kusini ambapo alifanyiwa upasuaji.

Kwa mujibu wa wataalamu waliomfanyia upasuaji walishauri apumzike kwa muda wa wiki sita ambazo zinatarajiwa kukamilika Oktoba 21.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live