Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dube aanika siri ya 5-0 za Azam FC

Azam FC Dubeeeeeee Dube aanika siri ya 5-0 za Azam FC

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Azam gari lao limewaka kwani kwa sasa wanagawa vichapo kila timu inayokutana nayo kwani jana usiku iliinyoa KMC kwa mabao 5-0, huku mshambuliaji hatari wa timu hiyo kufunga mara mbili na kufunguka siri ya juu ya ushindi mfululizo wa timu hiyo na mzuka walionao kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara.

Azam ilipata ushindi kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa timu hiyo kumpiga mtu 5-0, kwani mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar pia iliinyoosha kwa idadi hiyo na kuandika rekodi ya kucheza mechi nne na kufunga mabao 16.

Mabao mengine ya Azam yaliwekwa kimiani na Gjibril Sillah, Feisal Salum na Ismail Gambo wa KMC alijifunga wakati akiokoa shuti la Kipre Junior aliyewavuruga kwenye mchezo huo wa jana kwa kuasisti pia mabao mawili yote yakiwa ya Dube.

Akizungumza na Mwanaspoti Dube amesema kwa sasa timu yao imerejea kwenye utulivu mkubwa na kila mchezaji amekuwa na mzuka mwingi ndio maana timu imekuwa ikipata matokeo mazuri tangu ilipopoteza mechi mbili mfululizo kwa mabao 3-2 na 3-1 kwa Yanga na Namungo mtawalia.

Azam iliifumua Mashujaa mabao 3-0 kisha kuilaza Ihefu kwa 3-1, kabla ya kuifumua Mtibwa 5-0 na kurudia kipiogo hicho jana usiku na kuifanya timu hiyo irejee kileleni ikifikisha pointi 25, moja zaidi na ilizonazo Yanga ambao hata hivyo ina michezo miwili mkononi kulinganisha na Azam iliyocheza 11 hadi sasa, Yanga ikicheza 9.

Dube, ambaye ni raia wa Zimbabwe amesema ndani ya kikosi chao kuna utulivu mkubwa umerejea na wameanza kuwa kikosi kimoja kinachocheza kwa malengo ya kifamilia.

Mshambuliaji huyo amesema baada ya hali ya kujiamini kurejea na kuanza kuzoea mafunzo ya kocha sasa wanataka heshima irudi kwa kuupigania ubingwa.

"Tumeanza kuwa sawa kwasasa timu yetu ni kama familia moja, hizi mechi tulizokuwa tunashinda zimerudisha kitu kikubwa kati yetu wachezaji na makocha," Debe amesema na kuongeza;

"Unaona Sasa kila mtu ana furaha makocha wanafurahia kazi na sisi tunafurahia umoja wetu kama wachezaji, hili linatufanya Sasa kuanza kufikiria kuhusu kupigania ubingwa wa Ligi."

Nyota huyo wa kimataifa wa Zimbabwe amesema kuimarika kwa Azam kutaendelea kuwa mwiba kwa timu pinzani zinazokuja mbele ya timu hiyo kwani wameutamani ubingwa baada ya kuukosa tangu 2014.

"Sio rahisi tena kuruhusu yaliyokuwa yanapita kwetu yarudi, tunataka kuendelea kushinda tuweze kufanikisha malengo ya timu yetu, tutashinda zaidi sio kwamba KMC ni wabovu hapana kinachoendelea timu yetu imekuwa bora kuliko tunaokutana nao," amesema nyota huyo aliyefikisha jumla ya mabao matano kwa sasa.

Chanzo: Mwanaspoti