Gumzo la mshambuliaji wa Azam, Prince Dube, aliyeamua kubwaga manyanga na kutaka kuachana na timu hiyo kabla ya mkataba kumalizika sasa limechukua sura mpya baada ya kupewa ofa.
Wakati wengi wakijiuliza staa huyo anakwenda wapi baada ya Mwanaspoti kuandika kuhusu ofa alizonazo, sasa imefahamika kuwa Yanga imeshapeleka ofa.
Iko hivi, Yanga inaelezwa kuwa imelipa kisasi kwa timu hiyo baada ya Azam kumchukua kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu uliopita, nayo sasa imemuandalia mkataba wa miaka miwili mshambuliaji huyo.
Dube aliyeifungia Azam mabao sita msimu huu, kwenye ligi amegoma kurejea klabuni hapo akishinikiza kuondoka kwa madai hana furaha na klabu hiyo iliyomleta nchini miaka minne iliyopita na juzi alionekana akiwa kwenye majukwaa ya Uwanja wa Benjamin Mkapa analindwa na mabodigadi kila upande akishuhudia mechi ya Azam ambayo ilishinda 2-1 dhidi ya Yanga.
Baada ya Dube kujiondoa kikosini akawafuata Azam akitaka kulipa fedha ili anunue mkataba wake huku matajiri hao wa Chamazi wakigomea kiasi hicho cha dola 150,000 na kutaka dola 300,000 sawa na zaidi ya Sh700 milioni.
Hata hivyo, Azam baadaye ikaweka bayana kupokea ofa mbili za mshambuliaji huyo, akitakiwa na Simba na Al Hilal ya Sudan, ingawa staa huyo wa Zimbambwe inaelezwa alizigomea klabu zote mbili akiendelea na msimamo wa kutaka kuwa huru.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Dube tayari ameshaandaliwa mkataba wa miaka miwili na Yanga ukiwa na maslahi ya kutosha.
“Dube ameandaliwa mkataba na Yanga, nadhani ndio klabu anayoitaka kuichezea hapo Tanzania, mkataba una vipengele vingi, kuna nyumba, gari lakini mshahara nao ni mnono sana, Azam wangemuacha tu kwani tayari wameshampa mkataba na hana furaha na maisha ya Azam.
“Ukiongea naye anakuwa mkali sana hataki kuisikia Azam wala klabu yoyote, ukiongea anasema anataka kucheza klabu ambayo ina tabia ya kuchukua makombe kwani anataka kuwa na mafanikio kokote anakokwenda,” alisema mmoja wa marafiki wa mshambuliaji huyo anayecheza nchini.
Inaelezwa walinzi waliokuwa wakimlinda Dube juzi wanatoka kwenye kampuni moja kubwa ya ulinzi binafsi (jina tunalo), inayomilikiwa na kigogo wa Yanga.