Straika nyota wa Azam FC, Prince Dube amesema hawana sababu ya kuangalia watakutana na nani lakini kitu kilichopo kwenye akili zao ni kuchukua taji la Kombe la Mapinduzi.
Azam kesho itakutana na Singida Fountain Gate katika mchezo wa robo fainali utakaopigwa saa 10 jioni ikiwa ni mechi ya tatu ya hatua hiyo.
Akizungumza nasi, Dube alisema kwenye mataji ambayo wanayapigania msimu huu ubingwa wa Mapinduzi pia umo kwenye hesabu zao na wanajua wanaanza mechi ngumu zaidi kuanzia leo.
Dube alisema sio tu Singida hawataki kumuacha salama yeyote watakayekutana naye baada ya kumalizana na Singida ili watinge fainali na kuchukua ubingwa huo.
Dube aliongeza ukiondoa wachezaji ambao wamekwenda timu za Taifa wao waliobaki wanajiona wanatosha kurudisha ubingwa huo wa sita kwenye makabati ya mataji ya timu hiyo pale Azam Complex Chamazi.
“Hakuna timu tunayoihofia kila timu tunaichukulia kwa uzito mkubwa ili tufikie malengo yetu kwa kuchukua ubingwa huu, tunajivunia kikosi chetu kipo sawasawa kutupa mafanikio haya. Huwezi kuchukua ubingwa kama hutathibitisha ubora wako kwa kucheza na timu ngumu, tupo tayari sio tu na Singida bali na yeyote atakayekuja mbele baada ya Singida,” alisema Dube.
Azam ina uwezekano wa kukutana na Simba kwenye mchezo wa nusu fainali endapo Wekundu wa Msimbazi wataing’oa Jamhuri na Wanalambalamba wakiitoa Singida mechi zote zikipigwa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.