Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Drogba ndani ya Suzuki ya Dk Mwankemwa

Drogba X Mwankemwa Drogba ndani ya Suzuki ya Dk Mwankemwa

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aliyekuwa daktari mkongwe zaidi wa tiba za wanamichezo nchini, Mwanandi Mwankemwa leo amehitimisha safari ya maisha yake hapa duniani na kuzikwa kwenye nyumba yake ya milele, jijini Dar es Salaam.

Mwankemwa analiliwa na wanamichezo. Kwa aliyebahatika kuzungumza naye hata kwa nusu dakika, anafahamu ni mtu wa aina gani. Ni muungwana licha ya ukubwa wa taaluma ya udaktari kichwani kwake.

Alikuwa msaada kwa wengi. Waliopata majeraha na waliotamani kujifunza na kufahamu lolote kutoka kwake. Hakuwa mchoyo wa elimu na kwenye nafsi yake alinyimwa kiburi kwa waliokuwa chini yake.

Kuna simulizi moja ambayo wengi hawaifahamu. Ni kuhusu Mwankemwa na Didier Drogba, ligendi wa soka kutoka Ivory Coast aliyewahi kutamba na timu ya taifa Ivory Coast na Chelsea ya Ligi Kuu England.

Ni hivi. Mwankemwa ana gari ndogo ya kizamani aina ya Suzuki na alipenda sana kuitumia gari hiyo.

Ilikuwa Januari 3, 2010 na timu ya taifa ya Ivory Coast ilikuja kuweka kuweka kambi fupi kujiandaa na Fainali za Mataifa Afrika zilizokuwa zinafanyika Angola, ikiwa na mastaa wake wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, huku mmoja tu ndiye aliyekuwa akicheza soka la nchini kwao.

Ivory Coast ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Drogba alikuwa ni mmoja wa mastaa waliokiwasha siku hiyo, huku wakati wote akiwa hapa alikuwa chini ya uangalizi wa daktari wa Chelsea, aliyefuatilia afya ya mshambuliaji huyo.

Hata hivyo, baada ya mchezo huo, mshambuliaji huyo alikuwa amepata maumivu ya nyama za paja kidogo na alimjulisha yule daktari wa Chelsea palepale uwanjani.

Baada ya kujulishwa hilo, yule daktari haraka alituma taarifa Chelsea England kisha akatafuta daktari mzuri wa tiba za wanamichezo akaletewa Mwankemwa na kujiridhisdha ni mtu sahihi.

Yule daktari wa Chelsea alimtaka Mwankemwa kuungana naye mpaka hoteli ya Kilimanjaro Kempinski ili kama kuna lolote litakalohitaji msaada wake asaidie kwa haraka na Mwankemwa alikubali. Hata hivyo, Mwankemwa hakupanda gari yao, aliongozana na msafara wa timu hiyo huku akitumia gari yake (Suzuki) hadi hotelini ilikoweka kambi timu hiyo.

Baada ya kufika hotelini, maelezo yalikuja haraka kutoka Chelsea na ilitaka Drogba afanyiwe vipimo na watumiwe ili wavisome na kutoa maelekezo mengine.

Ilivyokuwa sasa. Wakati wanataka kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hawakutaka nyota huyo wa Chelsea aonekane kwa watu na hivyo, waliangalia uwezekano wa haraka wa kufanikisha hilo, huku vipimo vyake vikitakiwa haraka na viongozi wa Chelsea ili kutoa maelezo mengine.

Ilibidi daktari huyo wa Chelsea alifanya maamuzi ya haraka na kushtua wengi baada ya kumwamuru Dorogba kupanda Suziki la Mwankemwa, huku yeye akitumia pia hilo hilo na safari ya Muhimili ikaanza na walipofika aliwaambia 'mbona tumefika vizuri, huku akimwangalia Mwankemwa na kumwambia "Gari lako linaonekana nje la zamani, lakini bado imara sana."

Baada ya vipimo kurudi baada ya dakika 46, safari ya kurudi hotelini ilitakiwa kuanza mara moja na majibu yaliyokuja yalisema Drogba hakuumia sana na kulikuwa na maelekezo ya namna ya kumfanyia matibabu na nyota huyo baada ya matibabu hayo alirudi katika hali yake.

Hata hivyo, baada ya matibabu yale, maofisa wa Ivory Coast waligoma nyota huyo ambaye ameshastaafu soka, asipande kwenye Suzuki na kuletewa gari jingine aina ya Toyota Land Cruiser.

Maamuzi hayo hayakumfurahisha daktari wa Chelsea na aliona kama wameidharau gari lile (Suzuki) ambalo ndilo lililomsaidia mshambuliaji huyo kuwahi kupata matibabu.

Asante Mwankemwa. Umeondoka umetuachia kumbukumbu hii nzuri ya Drogba, nyota mkubwa na aliyewahi kutamba duniani kwa soka lake, kutumia Suzuki yako. Hakika hata anayeisoma sasa, ataendelea kuishi na kumbukumbu hii.

Kapumzike Mwankemwa. Soka la Tanzania limepoteza mtu bingwa.

Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake tutarejea!!

Chanzo: Mwanaspoti