Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Didier Drogba ametoa wito wa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ili kuwalinda wachezaji wa soka nchini kwao Ivory Coast baada ya kifo cha mchezaji mmoja wakati wa mchezo wa ligi kuu.
Beki wa Racing Club d'Abidjan (RCA) Moustapha Sylla, 21, alianguka wakati wa mechi dhidi ya SOL FC Jumapili na kutangazwa kuwa amefariki alipokuwa akipelekwa hospitali, kulingana na klabu yake.
Video ya tukio hilo inamuonyesha Sylla akijikwaa kabla ya kupoteza fahamu na kuanguka chini bila na kuwafanya wachezaji wa upinzani kuomba msaada wa matibabu.
Rais wa RCA Logossina Cisse alimuelezea Sylla kama "nyota anayechipukia ambaye aliondoka mapema sana" huku Shirikisho la Soka la Ivory Coast (FIF) likiongoza sifa zake kwenye mitandao ya kijamii.
"Katika wakati huu wa maumivu na hisia, FIF inatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu, kwa wasimamizi na wachezaji wa RCA, pamoja na familia ya mpira wa miguu ya Ivory Coast," FIF iliandika kwenye Facebook.