Licha ya ushindi mzuri, kocha wa Rangers Giovanni van Bronckhorst amesema timu yake inahitaji kutulia na kuendelea kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili ya kushinda mechi ya marejeano na Borussia Dortmund katika mchezo wa Ligi ya Europa hatua ya 32.
Dortmund wakiwa nyumbani dimba la Signal Iduna Park, ilikubali kipigo cha goli 4-2 na Rangers ambayo kiungo mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Juventus Aron Ramsey anakipiga huko.
Kocha huyo raia wa Uholanzi anasema ndiyo ni ushindi murua lakini mchezo huo ni kama umechezwa nusu kipindi pekee.
“Bado hatujafuzu hatua inayokuja, kitu ambacho tunakihitaji zaidi. Tunahitaji kuwa na ubora zaidi ya hapa”, alisema kocha huyo.
Katika mchezo huo magoli ya Rangers yamefungwa na James Tavernier baada ya mapitio ya VAR, Alfredo Morelos kuongeza bao la pili kabla ya John Lundstram kufunga goli la tatu, magoli yote yakifungwa ndani ya muda mfupi.
Kiungo mkabaji wa England Jude Bellingham aliipa unafuu Dortmund kwa kufunga goli la kwanza kabla ya Raphael Guerreiro kufunga goli la pili kwa Dortmund ambao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga nyuma ya vinara Bayern Munich.
Matokeo hayo yanaifanya Rangers kwenda kwenye mchezo wa mkondo wa pili wakiwa na faida ya magoli mawili dhidi ya Dortmund ambapo pia watakuwa wanacheza dimba la nyumbani.