Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dortmund, Madrid Ubabe ni mwingi

Madris Vs Dortmund Dortmund, Madrid Ubabe ni mwingi

Sat, 1 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ile siku ndo leo. Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itapigwa huko Wembley, ambako Real Madrid na Borussia Dortmund zitaonyeshana kazi, katika mechi yenye kujuana ndani yake.

Ushindi kwa Dortmund utakomesha miaka 27 ya kulisaka taji hilo la kibabe Ulaya na hapo watakuwa wamebeba ubingwa wa pili, wakati Los Blancos yenyewe inasaka taji lake la 15.

Dortmund inayonolewa na Edin Terzic iliisukuma nje Paris Saint-Germain kwenye nusu fainali, wakati Los Blancos ya Carlo Ancelotti iliichapa Bayern Munich kwenye hatua hiyo ya nne bora.

Dortmund inarudi kucheza fainali kwenye uwanja huo, ambao miaka 11 iliyopita, ilimenyana na Bayern Munich na kupoteza 2-1. Marco Reus na Mats Hummels walicheza fainali hiyo na usiku wa leo Jumamosi, watakuwapo. Wataumizwa tena? Au wataibuka kidedea? Ngoja tuone.

Real Madrid, mabingwa mara 14, ambao wataingia uwanjani kusaka taji la 15, kwenye kikosi chao kuna kiungo Jude Bellingham, ambaye atakumbana na waajiri wake wa zamani, Dortmund.

Mchongo ndani ya kambi

Real Madrid haitakuwa na huduma ya beki wake David Alaba na kiungo Aurelien Tchouameni wanaosumbuliwa na maumivu na kipa Andriy Lunin mwenye hatihati kubwa, huku kocha Ancelotti akiwa na uhakika mkubwa wa mastaa wake Thibaut Courtois, Nacho Fernandez na Jude Bellingham. Toni Kroos anatarajia kuanza na Eduardo Camavinga na Federico Valverde kwenye kiungo, ambako Luka Modric ataanzia benchini, huku kwenye fowadi kutakuwa na Wabrazili, Rodrygo na Vinicius Junior. Joselu atangoja benchini licha ya kuwa shujaa kwenye nusu fainali.

Kwa upande wa Dortmund, madaktari wa timu hiyo walikuwa bize kuhakikisha wanawapa tiba na kupona ndani ya muda mastaa Ramy Bensebaini (goti), Julien Duranville (misuli) na Mateu Morey (ugonjwa). Kuna wasiwasi pia wa kuhusu straika, Sebastien Haller, ambaye anasumbuliwa na maumivu ya enka, lakini wanaamini watapata huduma bora kutoka kwa Niclas Fullkrug, Reus, Julian Brandt, Jadon Sancho na wakali wengine wenye uzoefu kama Emre Can na Sabitzer.

Jino kwa jino

Real Madrid na Dortmund zimeshakutana mara 14 kwenye michuano hiyo ya Ulaya, ambapo Los Blancos iliibuka na ushindi mara sita dhidi ya mbili za BVB.

Mechi yao ya hivi karibuni ilikuwa katika msimu wa 2017-18, huku ushindi wa mwisho kwa Dortmund kupata mbele ya Madrid ilikuwa kwenye matokeo ya 2-0 katika mechi ya pili ya robo fainali 2013-14. Lakini, yote hayo ni historia, kinachosubiriwa ni kipute cha usiku wa leo, nani atatoboa?

Vikosi tarajiwa;

Borussia Dortmund: Kobel; Ryerson, Hummels, Schlotterbeck, Maatsen; Sabitzer, Can; Sancho, Brandt, Adeyemi; Fullkrug

Real Madrid: Courtois; Carvajal, Rudiger, Nacho, Mendy; Valverde, Camavinga, Kroos; Bellingham; Rodrygo, Vinicius Junior.

Chanzo: Mwanaspoti