Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma Jiji yaihofia Ihefu

Dodoma Jiji Pic Dodoma Jiji yaihofia Ihefu

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji FC, Kassim Liogope, amesema kuwa mechi yao dhidi ya Ihefu inayotarajiwa kuchezwa Ijumaa ijayo, itakuwa ni ngumu kutokana na timu hiyo kuonja joto la kukaa mkiani, hivyo haitotaka kurejea tena ilikokuwa.

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya mechi hiyo, alisema wamejipanga vema kukabiliana na timu hiyo ambayo kwa sasa imekuwa tishio kutokana na kufanya usajili mzuri wa wachezaji wakubwa na wa kimataifa.

"Ihefu na sisi ni timu ambazo hatujaachana sana, ni ngumu sana kwenda kucheza na timu ambayo ilikaa chini kwa muda mrefu, haitokubali kutoka kule ilikotoka.

Hata sisi tulikaa nao kule chini, lakini wenzetu kwa sasa wapo juu kidogo, wamefanya usajili mzuri, nadhani mechi itakuwa nzuri sana," alisema Liogope.

Dodoma Jiji inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, Jamhuri Dodoma, ikiwa na machungu ya kufungwa mabao 2-1 Jumamosi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro.

Timu hiyo inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 24 kwa mechi 23 ambazo imecheza, hivyo kuwa moja kati ya timu zinazohitaji zaidi ushindi ili kujiondoa kwenye eneo hatari ambalo linaweza kusababisha kushuka daraja au kwenda kucheza mechi za mchujo ili kubaki au kushuka.

Timu zitakazomaliza nafasi ya 16 na 15 zitashuka daraja moja kwa moja na zitakazoshika nafasi ya 14 na 13 ligi itakapomalizika, zitakwenda kucheza mechi za mchujo na timu zitakazoshika nafasi za tatu na nne kwenye Ligi ya Championship, ili kupata timu zitakazobaki Ligi Kuu au kuteremka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live