Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma Jiji wapiga tizi kupitia Group la Whatsapp

Dodoma Jiji Pic Dodoma Jiji wapiga tizi kupitia Group la Whatsapp

Fri, 24 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama mpaka Aprili 7 mwaka huu, Dodoma Jiji inaendelea na mazoezi kupitia group la Whatsapp

Uongozi wa timu hiyo umetoa mapumziko ya siku tisa (9) kwa wachezaji wake na wiki ijayo itarejea kambini kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Coastal Union unaotarajiwa kufanyika Aprili 13 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa.

Dodoma Jiji inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo ikiwa na pointi 27 katika michezo 25 iliyoicheza mpaka sasa na imebakisha michezo mitano kumaliza ligi hiyo,miwili nyumbani (Coastal na KMC) na mitatu ugenini (Yanga,Namungo na Ruvu Shooting).

Msemaji wa timu hiyo Moses Mpunga alisema Kocha wa timu hiyo, Melis Medo ametoa program maalum kwa kila mchezaji kupitia group la Whatssap lengo likiwa ni kuhakikisha wachezaji wanarudi wakiwa na viwango vile vile baada ya mapumziko.

“Tunaamini wakiwa huko watajitunza na wataendelea na program ambazo kocha wetu amewapatia kupitia group letu la Whatssap ili wakirudi tusianze moja kwa sababu mara kadhaa tumekuwa tukiona viongozi na makocha wanapotoa ruhusa kwa wachezaji wanaporejea wanalazimika kuanza moja.

“Sisi changamoto yetu imekuwa sio kubwa kwa sababu kocha amekuwa akiendelea na project yetu na uzuri kocha bado yupo Dodoma wale ambao wapo Dodoma mara chache amekuwa akikutana nao kuweza kuwaongezea vitu,”amesema Mpunga.

Msemaji huyo alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanashinda michezo miwili ya nyumbani dhidi ya Coastal na KMC ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia katika ligi kuu. Katika hatua nyingine,Msemaji wa Serikali,Gerson Msigwa amesema Dodoma Jiji bado wana nafasi ya kupambana kuhakikisha hawashuki daraja.

“Dodoma Jiji haijawa na matokeo mazuri,na mimi sina namna nipo Dodoma na Serikali ipo Dodoma ila timu yangu ni Majimaji,kinachotakiwa ni kupambana wasishuke daraja,” alisema Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

Chanzo: Mwanaspoti