Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma Jiji waanza mzunguko wa pili na ushindi Jijini Mbeya

Mbeya City Pic Kikosi cha Dodoma Jiji

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dodoma Jiji imelipa kisasi baada ya kuwakanda Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza katika duru la pili ambapo City waliingia dimbani wakikumbuka ushindi wa 3-1 walipocheza na wapinzani hao katika uwanja wa Liti mkoani Singida.

Mabao katika mchezo wa leo yamefungwa na Christian Zigah dakika ya 17 na Zidane Sereri dakika ya 78 huku la kujifariji kwa Mbeya City likifungwa na Eliud Ambokile dakika ya 90.

Hizi ni dondoo za mtanange huo.

Huu unakuwa ushindi wa tatu mfululizo kwa Dodoma Jiji baada ya ule dhidi ya Coastal Union 1-0 na Ruvu Shooting mabao 2-1 na kuifanya timu hiyo kupanda nafasi ya 11 kwa pointi 18.

Mbeya City imefikisha mechi saba kati ya kuni ilizocheza uwanja wa Sokoine bila ushindi ikiwa ni sare sita, kupoteza miwili na ushindi miwili na kubaki nafasi yake ya nane kwa pointi 20.

Kinara wa mabao wa Mbeya City, Sixtus Sabilo (saba) anafikisha mechi sita mfululizo sawa na dakika 540 bila kufunga bao tangu alipofanya hivyo Novemba 13 wakati wa sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union.

Pia City inafikisha dakika 630 bila kuonja ushindi tangu ilipoikamua Namungo 2-1 Novemba 4 katika uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya sita, ambapo kila upande umeshinda mechi mbili, sare mbili na kupoteza moja moja huku jumla ya mabao 14 yakifungwa kwenye mechi hizo.

Kocha Msaidizi wa timu Dodoma Jiji, Kassim Liogope amesema siri ya ushindi wa leo ni mbinu walizokuja nazo kuwaficha washambuliaji watukutu wa Mbeya City, Tariq Seif na Sixtus Sabilo.

"Tulijua mechi ni ngumu kutokana na Mbeya City kuwa na washambuliaji bora, tukaamua kutowaruhusu kutembea na mpira tunashukuru imetusaidia kuondoka na alama tatu" amesema Liogope.

Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima amesema kutopata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani ni moja ya matokeo ya mpira japokuwa inawaumiza sana.

"Hawa ndio wachezaji wanaotupa raha muda mwingine, sisi tunatimiza wajibu wetu lakini ndio mpira ulivyo sare zimekuwa nyingi ila tunaweza kushinda nje ya Sokoine" amesema kocha huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live