DodomaJiji itawakosa wachezaji watano katika mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam katika mtanange unaotarajiwa kufanyika kesho saa 1 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Timu hiyo inashika nafasi ya 11 ikiwa na alama 32 huku Azam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43 zote zikiwa zimecheza mechi 28.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo June 24,2022 kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Azam, Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Mohammed Muya amewataja wachezaji atakaowakosa ni Abubakari Ngalema, Omary Kanyoro, Cleophace Mkandala, Omari Nassoro na Issa Abushehe.
Amesema wachezaji hao waliumia katika michezo iliyopita ya Ligi na wanaweza wasicheze pia katika mchezo wa mwisho Juni 29 dhidi ya KMC.
Muya amesema mandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamika na watahakikisha wanapata matokeo ili kukwepa kushuka daraja au kucheza Play off.
"Hatupo katika nafasi nzuri ni lazima tupate matokeo ili tusishuke na tusiende katika play off," amesema Muya.
Kwa upande wake nahodha wa Dodoma Jiji, Mbwana Kibacha amesema morali ya wachezaji ipo juu na watahakikisha wanapata matokeo katika mchezo huo.
"Ni mechi ambayo imebeba hatma yetu tunatakiwa kubaki daraja hivyo ni lazima tucheze kwa tahadhari na tupate matokeo, tupo tayari kuitetea timu yetu," amesema Mbwana.
Katibu wa Chama Cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA), Mweli Hamsini amesema mandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamika na kipute hicho kitapigwa saa 1 usiku.