Katika kuboresha kikosi msimu ujao Dodoma Jiji FC imeanza mazungumzo na kiungo wa Coastal Union, Gustapha Simon anayeelezwa anataka kuondoka klabuni.
Simon aliyewahi kuitumikia Dar City na Young Africans kwa nyakati tofauti anataka kutafuta changamoto sehemu nyingine licha ya viongozi wa timu hiyo kumshawishi ili abaki kwa msimu ujao.
Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Fortunatus Johnson amesema baada ya msimu kumalizika tayari walishapokea ripoti ya benchi la ufundi na kilichobaki ni kuifanyia kazi.
“Kinachoendelea ni tetesi ila tutakapokamilisha usajili tutauweka wazi, hivyo tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wachezaji hadi tutakapofikia muafaka,” amesema.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omary Ayoub amesema wachezaji wote ambao wataachana nao ni wale ambao hawakupata muda mwingi wa kucheza ila kila aliyekuwa muhimu watampigania kubaki.
Ikiwa dili hilo litakamilika Gustapha utakuwa usajili wa pili Dodoma Jiji msimu ujao kwani inafahamika kuwa aliyekuwa winga wa Polisi Tanzania, Iddi Kipagwile amesajiliwa na klabu hiyo ya jijini Dodoma.