Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma Jiji: Tutawaheshimu Prisons

Dodoma Jiji Watembeza Mkwara Dodoma Jiji: Tutawaheshimu Prisons

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pamoja na kiwango bora walichoonesha msimu huu katika Ligi Kuu, lakini Dodoma Jiji imesema haitaidharau Tanzania Prisons badala yake itapambana kuendeleza ushindi na kujiweka pazuri kwenye msimamo.

Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya sita kwa pointi 15, inatarajia kuwa kibaruani kesho Jumatano kuwabili Maafande hao wakikumbuka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Singida Fountain Gate kwa mabao 2-1 walipocheza nyumbani.

Hata hivyo timu hizo zinakutana ikiwa Prisons haijawa na mwenendo mzuri kutokana na kucheza mechi 10 na kushinda moja, sare nne na kupoteza mitano na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi saba.

Kutokana na matokeo hayo yasiyoridhisha, tayari imeachana na aliyekuwa kocha mkuu, Fred Felix 'Minziro' na kesho itakuwa chini ya kocha mpya, Ahmad Ally ambaye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union aliishuhudia akiwa jukwaani wakati wakilala bao 1-0 kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.

Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope amesema mchezo huo wanauhitaji japokuwa wanafahamu ugumu utakaokuwapo kutokana na wapinzani walivyo.

"Tunaipa ukubwa sana mechi hii kwani ni rahisi kucheza na timu ya juu kuliko kukutana na ya chini, Prisons tunaifahamu mpira wake wa nguvu tumejipanga na vijana wako fiti na tayari kushinda mechi hiyo ukizingatia tumetoka kupoteza" amesema Liogope.

Nahodha wa timu hiyo, Emanuel Martin amesema maelekezo waliyopewa na benchi la ufundi kilichobaki ni wao kufanyia utekekezaji akieleza kuwa waliumizwa na matokeo ya mchezo uliopita hivyo kesho ni ushindi.

"Tumekuwa na muda wa kutosha kujiandaa na hata Mbeya tumefika mapema kuzoea hali ya hewa, aliyejiandaa atashinda na mashabiki wetu wawe na matumaini kwmaba kesho tunaenda kupata pointi tatu," amesema Martin.

Naye staa wa Prisons, Hamis Mcha amesema baada ya kusota kwa muda mrefu bila ushindi kesho chini ya kocha wao mpya wanaenda kuianza safari mpya ya ushindi na kujinasua nafasi za mkiani.

"Tumefanyia kazi makosa chini ya kocha wetu mpya, huenda kesho ikawa siku njema kwetu katika kuondokana na matokeo yasiyoridhisha,  tunachoomba mashabiki waje kwa wingi" amesema Mcha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live