Wafanyabiashara wa zao la zabibu wamechangamkia fursa ya uwepo wa mechi ya Dodoma Jiji na Simba kwa kuwauzia bidhaa hiyo mashabiki wanaofika uwanjani hapo.
Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa saa 1 usiku katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa. Wajasiriamali hao wanawauzia mashabiki wanaofika uwanjani hapo kukata tiketi kwa ajili ya kuingia uwanjani.
Mfanyabiashara Neema Jaku amesema kutokana na mechi hiyo kuleta mashabiki wengi ameamua kuzifuata zabibu katika Kijiji Cha Mpunguzi na kuwauzia mashabiki hao.
"Mpaka sasa nimeuza kama Sh 20,000 nafurahi kwa sababu familia leo itafurahi, nimepata hela," amesema. Naye Ashura Juma amesema kutokana na mashabiki wengi kutokea Dar ameamua kufanya biashara hiyo. Amesema tayari amemaliza beseni lake alilokuja nalo uwanjani na sasa anasubiria mechi ifike usiku ili aangalie kwenye TV kwani hana uwezo wa kukata tiketi.