Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dodoma Jiji, Azam vita nzito

Azam FC Mbeya Ligi.jpeg Dodoma Jiji, Azam vita nzito

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Utamyu wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena kwenye mechi za raundi ya 19 na mapema jioni, Tabora United itakuwa wenyeji wa Coastal Union na usiku Azam itaialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex, mechi inayotolewa macho na mashabiki wa soka.

Tabora inaingia katika mchezo huo utakaopigwa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora ikiwa na presha zaidi kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Goran Kopunovic ambaye hajashinda katika mechi nane mfululizo za Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar 2-1, Desemba Mosi mwaka jana.

Kwa upande wa Coastal imekuwa na mwenendo wa matokeo mazuri kwani tangu ilipofungwa mabao 2-1 na Singida Fountain Gate Novemba 27, mwaka jana haijapoteza, ikicheza mechi sita mfululizo na imeshinda tano na sare moja.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliisha kwa suluhu, Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Septemba 29, mwaka jana. Kocha Mkuu wa Tabora, Kopunovic alisema, licha ya presha iliyopo kwake katika timu hiyo ila hana hofu juu ya hilo kwani anachoendelea kukifanyia kazi ni kuandaa wachezaji vizuri kuanzia suala la kisaikolojia na kutumia nafasi vizuri.

Kwa upande wa Azam inahitaji kuendeleza ushindi baada ya mechi ya mwisho kushinda bao 1-0, dhidi ya Singida huku Dodoma Jiji ikiwa haijashinda michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara tangu ilipoifunga Ihefu 1-0, Desemba 18, mwaka jana.

Huu ni mchezo wa nane kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara na saba iliyopita Azam FC imeshinda minne wakati Dodoma Jiji imeshinda mara moja, huku sare zikitoka miwili na mara ya mwisho zilitoka suluhu Oktoba 3, mwaka jana.

Azam itashuka uwanjani ikitioka kucheza mechi tatu za ugenini na iliambulia pointi tano ikiwamo ushindi wa mechezo uliopita dhidi ya Singida Fountain Gates na sare mbele ya Tabora United na Tanzania Prisons, lakini ikikosa huduma za nyota wake kadhaa walio majeruhi.

Chanzo: Mwanaspoti