Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Abbas aongoza mapokezi Serengeti Girls

Sere Warudi.jpeg Kikosi cha Serengeti Girls kikiwasili

Sun, 23 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbas ameongoza mapokezi ya timu ya taifa ya wasichana chini ya miaka 17 (Serengeti Girls).

Timu hiyo imewasili nchini mchana huu ikitokea India kwenye fainali za kombe la dunia kwa umri wao, ambako walitolewa katika robo fainali na Colombia kwa kipigo cha mabao 3-0.

Katika mapokezi hayo yaliyoshereheshwa na kikundi cha ngoma, msafara wa timu hiyo ulitoka uwanja wa ndege kwa king'ora na kwenda moja kwa moja kwenye uwanja wa Mkapa, ambako kuna mechi ya Ligi ya Simba na Yanga.

Mapema kabla ya kuondoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, kocha mkuu timu hiyo, Bakari Shime alisema hatua ambayo kikosi hicho imefika ni kubwa.

"Kama benchi la ufundi, tumejifunza vingi, wachezaji pia na uongozi, ripoti yangu itaeleza ni wapi tumejikwaa.

"Lakini kikubwa ni kujipanga ili kufuzu tena msimu ujao," amesema. Naibu waziri wa michezo, Pauline Gekul amesema hatua waliyofika Serengeti si ya kuibeza.

"uwekezaji mdogo tuliouweka umetufikisha robo fainali, tulipambana dhidi ya Colombia, ingawa changamoto ilikuwa ni mvua iliyonyesha kwenye mechi.

"Hakuna tunachowadai hawa vijana wetu, morali yao imetufikisha hatua hii na tunaamini ipo siku tutashinda kombe hili.

"Tuliyojifunza kama wizara tumeyachukua na huu ni mwanzo mzuri kwenye mashindano haya," amesema. Rais wa TFF, Wallace Karia aliomba wadau kuwekeza kwenye soka la wanawake akibainisha kwamba mipango yao ni kuona timu hiyo inafuzu kwa mara nyingine msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti