Licha ya kuhusika kwa mabao sita kati ya 33 yaliyofungwa na Yanga katika michezo 19 iliyocheza timu hiyo, beki Djuma Shaaban amefunguka na kuweka wazi kuwa bado hajaridhishwa na kiwango chake ndani ya timu hiyo.
Djuma amefunga mabao matatu na kuasisti tatu, aliliambia Mwanaspoti anafurahia maisha ndani ya Yanga kutokana na timu kupata matokeo lakini uwezo wake haujafikia asilimia 100.
“Kwani timu inapata matokeo ndio maana tunaonekana bora, lakini kwa upande wangu bado sijafanya kile mashabiki na uongozi wangu walikusudia kutoka kwangu muda bado upo nitaendelea kufanya kwa ubora zaidi,” alisema Djuma na kuongeza;
“Yanga ina wachezaji wengi wazuri na wenye uchu ya mafanikio ndio wamekuwa wakinizibia upungufu nilionao, natamani kuwa bora zaidi ya hapa nilipo na hilo linawezekana ni suala la muda tu.”
Akizungumzia juu ya upigaji penalti ndani ya Yanga na kufanikiwa kupata zote tangu alipoanza dhidi ya Ruvu Shooting ilipoibuka na ushindi wa 3-1 na juzi dhidi ya Azam, alisema habahatishi ni kazi aliyoizoea tangu akiwa AS Vita.
“Suala la kupiga penalti sijaanza Yanga ni jukumu maalum nililopewa tangu nikiwa Vita, hivyo nilikuwa nalifanyia mazoezi kabisa na sasa nimelizoea sikumbuki nilikosa lini mara nyingi nimekuwa nikipata,” alisema Djuma na kuongeza:
“Penalti haina mwenyewe ni kujiamini na kupiga ukiwa na akili kwamba timu nzima wewe ndio umeibeba ukikosa umewaangusha wachezaji na benchi la ufundi.”