Wakati mashabiki wa Young Africans wakisubiri kwa hamu fujo za usajili mpya ndani ya kikosi chao, timu hiyo iliyopata mafanikio makubwa msimu uliopita inaendelea kumeguka kutokana na nyota wengine kutajwa kuondoka.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu tayari wameshampoteza kocha Nasreddine Nabi aliyewapa mafanikio makubwa kwa kutwaa mataji sita, mawili ya Ligi, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Wakati maumivu ya kumkosa Nabi yakiwa bado mioyoni mwa Mashabiki na Wanachama, taarifa zinaeleza kuwa Beki Djuma Shaban na Kiungo Yannick Bangala wanaweza kuondoka ndani ya kikosi hicho.
Nyota hao ambao wamebakiza mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja, wanatajwa kuondoka kikosi hapo, huku ikitajwa kuwa kuna usajili mkubwa utafanyika kuziba nafasi nao.
Kupitia vyanzo mbalimbali ndani ya Young Africans imefahamika kuwa Djuma aliuomba uongozi kuondoka kikosini akiweka wazi kuwa anataka kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya Young Africans.
Wakati ombi lake likiwa bado halijajibiwa kuna tetesi kuwa Young Africans ipo kwenye mazungumzo na beki wa ASEC Mimosas, ambaye inaamini ataweza kuziba nafasi ya Djuma.
Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema kila mchezaji ambaye wamepanga kumpa mkataba watamtangaza kupitia kurasa za Mitandao ya Kijamii za Klabu, hivyo Wanayanga wanatakiwa kuwa wavumilivu.
Kamwe amesema kikosi chao kimerejea salama nchini kutokea Malawi kilipokuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Nyasa Big Bullets, ambao ulichezwa juzi Alhamis (Julai 06) na kumalizika kwa suluhu.
Amesema wanashukuru Mungu wamerejea nchini salama baada ya kufanikiwa kuonyesha mchezo mzuri licha ya winga Denis Nkane kupata majeraha yaliyotokana kuumia baada ya kugongana na beki wa Nyassa Big Bulltes.
Hadi sasa, Young Africans imefanya usajili wa mzawa Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate FC ikiwaacha wachezaji watano.